Faida 7 za Kuwa na Uvumilivu Unazotakiwa Kuzifahamu

 



Maisha yana milima na mabonde, kipindi cha raha na shida. Katika kipindi cha shida au wakati mtu anapokutana na changamoto swala la uvumilivu linahitajika sana, tena sana.

Kukosa uvumilivu kumewafanya wengi kushindwa kufanya maamuzi sahihi na kujikuta wakitumbukia kwenye shida zaidi. Haijalishi unapitia magumu mengi kiasi gani, kuvumilia ni lazima.

Ikiwa unataka kujifunza faida au umuhimu wa uvumilivu, basi fahamu faida 7 za uvumilivu katika maisha yako.

1. Hukuwezesha kufanya maamuzi sahihi

Ndani ya uvumilivu kuna subira, ikumbukwe kuwa wahenga walisema subira yavuta heri. Hii ina maana kuwa kufanya maamuzi mara ukutanapo na changamoto kunaweza kukusababishia kufanya maamuzi yasiyo sahihi.


Kwa mfano hebu fikiri mtu ameachwa na mchumba wake ghafla naye mara moja anataka kupata mwingine hapo hapo; ni wazi kuwa atatumbukia kwenye kupata mtu mwingine atakayemlaghai tena.

Hivyo ni muhimu kusubiri na kuvumilia hadi wakati sahihi ili ufanye maamuzi sahihi.

2. Huwezesha kufikia malengo

Uvumilivu ni swala muhimu sana katika safari ya kutimiza malengo yetu. Katika safari ya kufikia malengo yetu kuna vikwazo na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji uvumilivu ili kuzivuka.

Watu watakupinga, wengine watakuchukia, unaweza kupata hasara, n.k. haya yote yanahitaji uvumilivu ili uweze kuyavuka na kufikia malengo.

3. Hukufanya jirani au rafiki mwema

Hebu fikiri una rafiki au jirani mgomvi au mbaya; wewe nawe ukikosa uvumilivu ukimlipa baya kwa baya moja kwa moja utashindwa kuishi naye.

Kwa njia ya kuwa mvumilivu utaweza kuvumilia na kutafuta hekima na busara ya kuishi na watu kama hao.

4. Hukuwezesha kufikia muda sahihi

Kila jambo maishani mwetu limefungwa kwenye muda.

Kuna muda sahihi wa kufanya jambo fulani na muda ambao siyo sahihi; hivyo uvumilivu utakuwezesha kufikia muda sahihi ambao utakuwezesha pia kufanya maamuzi sahihi kwa muda sahihi.

Kwa mfano mabinti wengi hukosa uvumilivu kwenye masomo yao na kuishia kupata mimba au kuolewa kabla ya kukamilisha masomo yao. Hivyo katika jambo lolote uvumilivu ni swala la muhimu.

5. Hukuwezesha kupata watu au vitu sahihi

Inawezekana leo huna pesa, huna kazi, huna chakula, huna nyumba au mahitaji yako ya msingi, lakini kumbuka kuwa wakati mwingine vitu au watu huja kulingana na muda, hivyo kukosa uvumilivu kutakusababisha ukose vitu au watu hao.

Wapo watu waliovumilia kuishi maisha ya chini wakiwa hawana nyumba, kazi, gari au hata mwenzi wa maisha; lakini kutokana na uvumilivu huo waliweza kufikia wakati stahiki na kuvipata vitu hivyo.

6. Hukufundisha upande wa pili wa maisha

Kama nilivyotangulia kusema kuwa maisha yana pande mbili, upande wa raha na upande wa shida. Uvumilivu huhitajika zaidi wakati wa shida; hivyo huwezi kuwa mvumilivu kama hupitii changamoto mbalimbali.

Unapokuwa mvumilivu unapata nafasi nzuri ya kujifunza upande wa pili wa maisha, kama ulikuwa umezoea kucheka kila wakati utatambua kuwa kuna wakati wa huzuni, kama ulizoea kupata kila wakati utatambua kuwa kuna wakati wa kukosa.

Hili pia litakuwezesha kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na upande wa pili wa maisha.

7. Hukujengea ushuhuda

Huwezi kuwa na ushuhuda mzuri wa mafanikio tu kwa maisha yako yote; ushuhuda mzuri na unaogusa maisha ya wengine ni ule wa namna ulivyoishi pande zote za maisha, yaani wakati wa raha na wakati wa shida.

Kwa kuwa na uvumilivu utaweza kutengeneza ushuhuda mzuri ambao kila atakaeusikia baadaye atajifunza na kuhamasika zaidi. Hili ni kutokana na sababu kuwa watu wataona ulivyokutana na changamoto lakini hukukata tamaa bali ulivumilia hadi mwisho.

Neno la mwisho

Natumaini umeona wazi kuwa uvumilivu hauepukiki kwenye maisha yetu kwani kuna changamoto na vikwazo mbalimbali ambavyo tunapaswa kuvivumilia.

Ukichunguza kwa karibu historia ya watu waliofanikiwa sana utagundua kuwa wamevumilia mengi hadi wakafikia malengo na mafanikio waliyonayo.

Post a Comment

0 Comments