Magufuli aahidi kujenga barabara ya Makofia, Mlandizi Vikumburu


Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. John Magufuli amesema kuwa atajenga barabara ya Makofia, Mlandizi mpaka Vikumburu wilayani Kisarawe.

Magufuli ametoa kauli hiyo katika mkutano wa Kampeni katika viwanja vya Mwanakalenge wilayani hapa, ambapo alisema ilani ya Chama hicho kwa miaka mitano ijayo imedhamilia kujenga kwa kiwango cha lami barabara mbalimbali.

"Barabara ya Makofia Vikumburu kilometa 148, Vikawe Kibaha kilometa 23, sanjali na ile itokayo Kibaha Chalinze nyumbani kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, hii inatokana na ujenzi wa barabara inayoanzia Kimara mpaka Kibaha", alisema Dkt. Magufuli.

Aidha amepongeza uwepo wa viwanda vilivyojengwa katika Mkoa wa Pwani ambavyo vimeokoa fedha nyingi za kununulia malighafi nje ya nchi, ambayo yametumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea kujengwa hapa nchini.


Awali Rais Mstaafu wa serikali ya awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa haoni hofu ya wagombea wa chama hicho ngazi za Urais, Ubunge na udiwani, huku akielezea sababu kubwa inatokana na serikali inayoongozwa na Magufuli imefanya mambo makubwa.

"Chama chetu chini ya uongozi wako umefanya mambo mengi mazuri, wagombea ubunge wameelezea vizuri mambo makubwa yanayofanyika, Tanzania ya sasa sio niliyokuachia mwaka 2015, tumepiga hatua kubwa ya kimaendeleo na nchi imetulia tutakulipa kwenye boksi la kura Oktoba 28," alisema Jakaya.

 Nao wagombea Ubunge Ridhiwani Kikwete, Muharami Mkenge na Michale Mwakamo wamezungumzia kazi kubwa iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya tano inayoishia ukingoni, huku wakielezea matarajio yao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

"Niwaombe wana-Bagamoyo ikifika Oktoba 28 tujitokeze kwa wingi kuwapigia kura wagombea wanaotokea chama chetu, ili kwa pamoja tukaiendeleze kazi kubwa iliyofanyika kipindi kinachoishia," alisema Mkenge.

 

Post a Comment

0 Comments