China leo imeituhumu Marekani kwa uuzaji wa silaha kinyume cha sheria na kuingilia kati masuala ya nchi zengine baada ya Marekani kutishia kuiwekea vikwazo nchi yoyote itakayofanya biashara ya silaha na Iran baada ya marufuku ya Umoja wa Mataifa kwa taifa hilo kuisha.
Wizara ya mambo ya nje ya China imesema haya baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kutoa onyo la Iran kuuziwa silaha na nchi yoyote duniani. Zhao Lijan ni waziri wa mambo ya nje wa China.
"Ni Marekani inayouza silaha kinyume cha sheria kila mahali, inatumia biashara za kijeshi kwa ajili ya siasa za kikanda na inaingilia kati waziwazi masuala ya ndani ya nchi zengine. Marekani haina haki ya kuizungumzia China chochote kile.
"Alipoulizwa iwapo China sasa itaiuzia Iran silaha Zhao hakujibu swali hilo moja kwa moja ila akadai kwamba China itafanya biashara za kijeshi kulingana na sera yake ya kuuza silaha nje ya nchi na majukumu yake ya kimataifa.
