Mwambe aahidi kufufua mfuko wa maendeleo ya Elimu Masasi ( MEFU)



Na Hamisi Nasri, Masasi.

MGOMBEA ubunge jimbo la Masasi mjini kwa chama cha Mapinduzi(CCM) Geofrey Mwambe amewahakikishia wananchi wa jimbo hilo kuwa iwapo akichaguliwa kuwa mbunge atafufua mfuko wa maendeleo ya elimu Masasi (MEFU) ili kurejesha hadhi ya kiwango cha elimu kwa kizazi kilichopo wilayani humo.  

Mwambe aliyasema hayo jana mjini Masasi wakati wa mkutano wake wa kampeni wa kuomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo, mkutano ambao aliufanya katika kata ya Napupa ambapo pia alitumia fursa hiyo kumuombea kura raisi,Dkt.John Magufuli na mgombea udiwani wa kata hiyo, Sospeter Nachunga.   

Alisema iwapo akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Masasi moja jambo ambalo pia atalifanyia kazi kulitekeleza ni pamoja na kufufua ule mfumo wa elimu Masasi ambao ulikuwapo katika miaka ya 1990 na baadae mfuko huo ulikufa ghafla na kupelekea baadhi ya changamoto za sekta ya elimu Masasi kukwama katika kuzitatua.   

Alisema bado hafurahishwi na hali ya maendeleo iliyopo ndani ya jimbo hilo hasa kwa upande wa elimu pamoja na miundombinu ya barabara kwa sababu kwa hadhi ya Masasi na maendeleo yanayofanywa bado haiyendani, hivyo akichaguliwa kuwa mbunge lazima kuwe na kasi kubwa ya kimaendeleo inayoendana na hadhi ya wilaya ya Masasi.  

Mwambe alisema kwa upande wake kuhusu elimu ataanza na kufufua mfuko wa maendeleo ya elimu Masasi (MEFU) ambao mfuko huo uliasisiwa na baadhi ya wadau wa elimu wilayani Masasi katika miaka hiyo ya 1990 ambapo lengo lake lilikuwa ni kuwakutanisha wadau hao wa elimu ili kuweka mikakati madhubuti ya kuinua kiwango cha elimu wilayani Masasi na kwa wakati huo ulifanikiwa. 

“Mkinichagua kuwa mbunge wenu wa jimbo la Masasi na kama hamtajali nawahakikisheni nitafufua mfuko wa elimu Masasi…mfuko huu kwa miaka ile ulikuwa na tija sana katika sekta ya elimu hadi ulifanikiwa kuanzishwa kwa shule ile ya sekondari MEFU ambayo sasa inaitwa shule ya Masasi kutwa naombeni kura ili tusaidiane kuinua elimu kwa watoto wetu,”alisema Mwambe    

Alisema kwa upande wa miundombinu ya barabara atahakikisha akiingia bungeni bajeti ya wakala wa barabara za mjini na vijijini(TARURA) katika jimbo la Masasi kupita Halmashauri ya mji Masasi inaongezwa ili kuweza kuboresha barabara za mitaa kwa ufanisi zaidi.  

Mwambe alisema katika jimbo la Masasi lina jumla ya kata 14 hivyo mtandao wa barabara sio mkubwa, TARURA halmashauri ya mji Masasi imekuwa ilipangiwa jumla ya bajeti milioni 600 kwa mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara fedha ambazo ni hazitoshelezi hivyo akiingia bungeni bajeti hiyo atahakikisha inaongezwa zaidi. 

Alisema anatamani huduma zote za msingi ziwe zinapatikana katika jimbo la Masasi na kwamba yeye ameshawai kushika nafasi kubwa serikalini ikiwemo nafasi ya mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji nchini(TIC) na zingine nyingi hivyo atatumia uzowefu aliyonao kuituumia Masasi iweze kupiga hatua ya kimaendeleo.   

Awali akimkaribisha mgombea huyo.katibu wa CCM wilaya ya Masasi,Shaibu Mtawa alisema chama cha mapinduzi kinaendelea kufanya kampeni zake za ubunge na udiwani katika majimbo yote matatu yaliyopo wilayani Masasi ambayo ni Ndanda,Masasi mjini na Lulindi na kwamba zote zimekuwa za ustarabu.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items