Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Butiama mkoani Mara Jumanne Sagini amewaahidi Wakazi wa Kijiji cha Mwanzaburiga Kata ya Kukirango kutatua kero ya mimba za utotoni pindi atakapo apishwa.
Hayo ameyasema mapema hii leo katika mkutano wa wake wa kampeni kuwa moja kati ya kero kubwa alizopokea katani hapo ni watoto kuzaa watoto ambao wengi wao ni wanafunzi walioachishwa masomo kutokana na kurubuniwa kwa hali kwa kifedha pia ikiwemo lifti za mara kwa mara za waendesha pikipiki.
"Kwa wale wanaume wenye tabia ya kujihusisha kwenye mapenzi na binti na mwanafuzi shule kisheria ni kosa la ubakaji na adhabu yake ni miaka 30 jela, ukiona binti amekuvutia na sare zake za shule kamshonee mkeo na sio kwenda kumuachisha masomo mnaharibu ndoto za kizazi cha leo," amesema Sagini.
Nawaomba wazazi kuweni karibu na watoto wenu wa shule muwape elimu juu madhara ya kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo na wajifunze kusema hapana pale waonapo viashiria vya ushawishi.
Aidha amewaomba wakazi wa kijiji hicho kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari pamoja na bweni kwa lengo la kupunguza na kudhibiti tatizo la mimba kwa wanafunzi.