Rais wa Marekani Donald Trump amemkosoa vikali daktari mkuu wa magonjwa ya kuambukizwa Marekani, Anthony Fauci, kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini humo.
Taarifa hizo zinasema akiwa mbele ya wafanyakazi wa timu yake ya kampeni ya uchaguzi, Trump alimfananisha Fauci na "janga".
Trump pia alisema mtaalamu huyo angesikilizwa, basi idadi ya raia wa Marekani waliokufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 ingekuwa kubwa zaidi. Trump na Fauci, ambaye ni mtaalamu katika kikosi chake cha kupambana na ugonjwa huo wamekuwa wakivutana juu ya namna ya kuudhibiti ugonjwa huo.
Virusi vya corona vimesababisha vifo vya watu 219,000 nchini Marekani, na kumpunguzia umaarufu kiongozi huyo wa chama cha Republican. Fauci amekuwa akipendekeza hatua kali kuendelea kuzingatiwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Trump hata hivyo anampinga na kusisitiza kwamba maambukizi yameshapungua kasi Marekani.
