Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa na maelfu wengine kutoroka eneo hilo baada ya wiki mbili za makabiliano.
Kuthibitisha hali ilivyo katika Jimbo la Tigray ni vigumu kwasababu huduma za mawasiliano zimekatizwa.
Mzozo huo umetokana na taharuki ya muda mrefu kati ya chama kikuu cha siasa katika eneo hilo,Tigray People's Liberation Front (TPLF) na serikali kuu ya Ethiopia.
Wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipohirisha uchaguzi kutokana na janga la corona, hali ya taharuki ilipanda kati ya pande hizo mbili. TPLF inachukulia serikali kuu ni batili ikadai kuwa Bwana Abiy hana mamlaka ya kuendelea kuongoza nchi.
Serikali inalaumu TPLF kwa kushambulia kambi ya majeshi kwa lengo la kuiba silaha, madai ambayo TPLF imepinga. Bwana Abiy alijibu madai hayo akisema kitendo hicho ni uhaini.
Ni yapi yanayojiri kwa sasa?
Siku ya Jumatano mamlaka za polisi katika serikali kuu zilitoa hati ya kukamatwa kwa maafisa 76 wa kijeshi, baadhi yao wanadaiwa kustaafu. Wanatuhumiwa kushirikiana na TPLF "kutekeleza uhaini", kwa mujibu wa shirika la AFP .
Akizungumza na BBC, Billene Seyoum - msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed - alipinga madai kwamba watu kutoka jamii yaTigrinya katika maeneo mengine nchini wanakamatwa kwa misingi ya kikabila.
Lakini amekiri kuwa watu kadhaa wanazuiliwa kwa kuwa wanachama wa kile alichokiita mtandao wa uhalifu.
Taarifa hizo zinakuja baada ya vikosi vya serikali kuteka miji ya Shire na Axum baada ya makataa ya siku tatu iliyotolewa na Waziri Mkuu Abiy kwa vikosi vya Tigray kujisalimisha kuisha siku ya Jumanne.
