Madaktari China wafungwa jela kwa ulanguzi wa viungo mwili

Watu sita ikiwemo madaktari kadhaa wamefungwa gerezani nchini China kwa kutoa viungo vya mwili kinyume cha sheria kwa watu waliokufa kutokana na ajali, vyombo vya habari vya eneo vimesema.


Kundi hilo lilikuwa limelaghai familia za waliokufa kuwa wanachangia rasmi viungo vya mwili katika mashirika husika.


Kati ya mwaka 2017 na 2018 walitoa maini na figo kutoka kwa watu 11 katika hospitali ya Anhui.


China inakabiliana na upungufu wa viungo vya mwili na imekuwa na wakati mgumu kukidhi mahitaji ya raia.


Kulingana na taarifa za wenyeji, kundi la wanaotekeleza uhalifu huo ni pamoja na madaktari wa ngazi ya juu baadhi yao wakiwa walifanya kazi katika vitengo vya uagizaji wa viungo hospitalini.


Vyombo vya habari vya eneo vimesema kuwa walilenga waathirika wa ajali za barabarani au wagonjwa waliokuwa na matatizo ya kutoka damu kwenye ubongo katika kaunti ya Huaiyuan hospitali ya Anhui.


Mkuu wa hospitali katika chumba cha wagonjwa mahututi, Yang Suxun, alizungumza na familia ya marehemu na kuwauliza kama wangependa kuchangia katika utoaji wa viungo. Na familia ingetia saini kile ambacho baadaye kilibainika kuwa karatasi bandia za kukubali ombi hilo.


Na aliyekufa angetolewa hospitalini usiku wa manane na kuwekwa ndani ya gari lililoonekana kuwa gari la kubeba wagonjwa ambapo madaktari wangemtoa mwathirika viungo vyake vya mwili.


Viungo hivyo vingeuzwa kwa watu binafsi au katika hospitali nyingine ambazo wakuu wa genge hilo wangewasiliana huko kwa njia ya siri, kulingana na taarifa.


Na hatimaye ukweli ulijulikana pale kijana mmoja wa mwathirika alipoanza kuwa na mashaka nao.


Miezi kadhaa baada ya kifo cha mama yake 2018, Shi Xianglin aliangalia tena stakabadhi ilizopokea familia yake walipokubali kuwa mama yao anaweza kuchagia utoaji wa viungo vya mwili na kubaini mapungufu mengi tu - ikiwemo baadhi ya sehemu katika fomu ambazo hazikujazwa.


Pia akabaini kwamba hakukuwa na rekodi zozote za mchango wa viungo aliotoa mama yake ama kwa ajili ya mamlaka ya eneo au kituo cha uchangiaji wa viungo China kilichopo Beijing.


Alikiambia chombo cha habari cha eneo cha Dazhongwang kuwa alipomuuliza Yang kuhusu hilo, kwa haraka sana alipewa kiasi kikubwa cha pesa ili "kumnyamazisha".


"Hapo ndipo nilipojua kuwa kuna njama fulani inayoendelea," amesema Bwana Shi.


Na Bwana huyo akaamua kujulisha mamlaka husika.


Wanaume sita wanaohusika na ulanguzi huo wa viungo vya binadamu walisomewa mashtaka yao Julai mwaka huu kwa kosa la "kuharibu miili ya wafu kimaksudi" na kuhukumiwa kifungo cha kati ya miezi 10 na 28 gerezani.

Post a Comment

0 Comments