DC Tarime Awapa Onyo Wakulima Wanaodaiwa Mikopo ya Pembejeo, Ataka Wawajibishwe

 


Na Timothy Itembe, Tarime

TARIME, MARA – Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amewataka wakulima wa tumbaku waliokopa pembejeo kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati ili kuwezesha upatikanaji wa pembejeo kwa msimu wa kilimo wa 2026/2027.

Meja Gowele alitoa kauli hiyo Julai 21, 2026, wakati wa mkutano wa wakulima ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU) uliofanyika katika viwanja vya Kijiji cha Nyabitocho, Kata ya Mbogi, Wilayani Tarime. Mkutano huo ulijadili maendeleo ya kilimo cha tumbaku, uhai wa soko la zao hilo na utekelezaji wa mikopo ya pembejeo.



Alisema baadhi ya wakulima walikiuka mikataba waliyoingia kwa kuuza tumbaku nje ya mfumo rasmi wa masoko, jambo lililosababisha kushindwa kurejesha mikopo ya pembejeo waliyopewa.

"Uaminifu ndio mtaji. Watu waliingia mikataba, tukajiridhisha tumbaku ililimwa, ikavunwa, lakini badala ya kuifikisha kwenye soko rasmi, baadhi waliipeleka nchini Kenya. Fedha za pembejeo ni mali ya umma na lazima zirejeshwe kupitia AMCOS," alisema Meja Gowele.

Alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vinavyohatarisha mustakabali wa kilimo cha tumbaku na kuagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wadaiwa sugu.

"Ninamuagiza OCD kwa kushirikiana na WAMACU kuandaa mashitaka dhidi ya kila aliyekopa na kushindwa kulipa. Hatuwezi kuruhusu watu wachache kuharibu sekta ya tumbaku. Wapo waliochukua pembejeo za mkopo bila hata kuwa na mashamba na wakaenda kuziuza," alisema.

Pia aliwataka wakulima kuacha kutorosha tumbaku kwenda nje ya nchi, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaikosesha Serikali mapato muhimu yanayotumika kugharamia huduma za jamii na miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU), Samwel Gisiboye, alisema AMCOS zinazodaiwa zaidi ni Nyakonga, Itiryo, Sirari, Mwesu, Kubiterere na Mbogi.

Alisema wakulima kupitia vyama hivyo wanadaiwa mikopo ya pembejeo yenye thamani ya shilingi milioni 386.458.

Gisiboye alisema wakulima waliomaliza kulipa mikopo yao wameiomba Serikali kuwachukulia hatua wadaiwa wote ili kuhakikisha mfumo wa utoaji wa pembejeo unaendelea kuwa endelevu.

"Wakulima waliopata masoko mazuri na kuuza tumbaku yao wanapaswa kulipa mikopo yao kwa wakati. Fedha hizo ndizo zitakazowezesha kuagiza mbolea na pembejeo nyingine kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo," alisema.

Naye Afisa Kilimo wa WAMACU, Prosper Mwita, alisema chama hicho kina ushahidi unaothibitisha kuwa wakulima wengi walilima na kuvuna tumbaku, lakini baadhi yao walishindwa kuipeleka kwenye soko rasmi licha ya kufuatiliwa katika hatua zote za uzalishaji.

"Tumekuwa tukitembelea mashamba kuanzia hatua za vitalu, ukuaji wa mazao hadi uvunaji. Ushahidi wote tunao. Changamoto iliyojitokeza ni kwamba baadhi ya wakulima hawakuleta tumbaku yao kwenye soko rasmi baada ya kuvuna," alisema Mwita.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi