Kiongozi wa mpito wa mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya ameonyesha matumaini yake kuelekea mazungumzo yanayolenga kufanya maandalizi katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita.
Mazungumzo hayo ambayo yanatarajiwa kuanza hii leo katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis, yanafuatia miezi kadhaa ya utulivu nchini Libya.
Mwezi uliopita pande mbili zinazohusika katika mapigano nchini humo zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano na kufungua milango ya kurejea kwa uchimbaji wa mafuta ambao ni muhimu kwa uchumi wa nchi hiyo na kutilia kikomo vita vya kisiasa ambavyo vimedumu kwa miaka kadhaa sasa.
Libya ni nchi iliyodhibitiwa na wanamgambo ambao wanaunga mkono pande mbili kuu za kisiasa nchini humo ambazo ni serikali ya mjini Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na utawala wa mashariki mwa nchi hiyo unaoongozwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar.
