Waziri wa fedha wa Uturuki na mkwe wa Rais Recep Tayyip Erdogan ametangaza kujiuzulu. Berat Albayrak mwenye umri wa miaka 42, mume wa binti ya Erdogan, ameandika jana kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa anajiuzulu wadhifa wake kwa sababu za kiafya na angependa kuwa na muda zaidi wa kukaa na familia yake.
Aliteuliwa kuwa waziri wa fedha na hazina ya taifa Julai 2018, baada ya kuhudumu awali kama waziri wa nishati kwa karibu miaka mitatu.
Kujiuzulu kwake kunafuatia kufutwa kazi mwishoni mwa wiki kwa mkuu wa benki kuu Murat Uysal na nafasi yake kuchukuliwa na waziri wa zamani wa fedha Naci Agbal. Bado haijafahamika kama rais Erdogan atakubali ombi hilo.
Mwezi Aprili, waziri wa Mambo ya Ndani Suleyman Soylu alijiuzulu kwenye Twitter, na akabatilisha tangazo hilo katika saa kadhaa baada ya Erdogan kukataa kulikubali.
