Aliyekuwa rais wa Kosovo Hashim Thaci anatarajiwa kufikishwa leo mbele ya mahakama ya uhalifu wa kivita mjini The Hague kujibu mashitaka yanayotokana na vita vya miaka ya 1990 kati ya Kosovo na Serbia.
Thaci, mwenye umri wa miaka 52 alijiuzulu Alhamisi iliyopita na kusafiri hadi Uholanzi ambako aliwekwa katika jela ya Mahakama Maalumu ya Kosovo mjini The Hague.
Majajii, mwendesha mashitaka maalum na wafanyakazi wa mahakama hiyo wanatoka katika jamii ya kimataifa.
Thaci na watuhumiwa wengine watatu wameshitakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu, ikiwemo mauaji, mateso, kuwazuilia watu kinyume cha sheria, kutoweka watu na mateso, matukio yaliyofanywa kati ya Machi 1998 na Septemba 1999.
Thaci ameahidi kushirikiana na mahakama hiyo itakayoanza kikao chake leo mchana. Alikuwa mkuu wa kisiasa wa Jeshi la Ukombozi wa Kosovo - KLA, ambalo lilipigana na wanajeshi wa Serbia kwa ajili ya uhuru wa mkoa huo wa kusini katika vita vilivyowauwa zaidi ya watu 13,000.
