Nabii milionea nchini Malawi Shepherd Bushiri na mke wake Mary wamejisalimisha kwa polisi katika eneo lao la nyumbani baada ya kukwepa masharti ya dhamana nchini Afrika Kusini.
Wanandoa hao wamejisalimisha katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe, Jumatano asubuhi kulingana na mwanahabari wa BBC Nomsa Maseko.
Awali mwezi huu, waliachiwa kwa dhamana na mahakama moja nchini Afrika Kusini baada ya kushtakiwa kwa makosa ya ulaghai na utakatishaji wa pesa.
Awali, muhubiri huyo alisema kuwa alitaka kutakasa jina lake.
Bwana Bushiri aliwaambia wafuasi wake katika mitandao ya kijamii Jumamosi kuwa uamuzi wake wa kukiuka dhamana ni kwasababu alipokea vitisho vya kifo.
Muhubiri huyo pia alishtumu Afrika Kusini kwa kushindwa kuwapa ulinzi.
Afrika Kusini ilikuwa imeanza mchakato wa kutaka warejeshwe nchini humo na Jumatatu ikatoa kibali cha kukamatwa kwake.
