Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema serikali ya Marekani na Ulaya zinahitaji kufanya kazi pamoja kushughulikia vitendo vilivyoongozwa na Uturuki katika Mashariki ya Kati miezi michache iliyopita.
Pompeo ameliambia gazeti la Ufaransa, Le Figaro kwamba Rais Emmanuel Macron na yeye, wamekubaliana kwamba vitendo vya hivi karibuni vya Uturuki vimekuwa vikali sana.
Pompeo anazungumzia hatua ya Uturuki kuiunga mkono Azerbaijan katika mzozo wa Nagorno-Karabakh, pamoja na shughuli za kijeshi nchini Libya na katika Bahari ya Mediterania.
Mwanadiplomasia huyo wa Marekani amesema Ulaya na Marekani zinapaswa kushirikiana kumshawishi Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kwamba vitendo kama hivyo havina maslahi kwa watu wake.
