Waziri anayehusika na masuala ya Afya Dr. Joyce Moriku Kaducu ametangaza kuwa serikali itachukua jukumu la kutibu waliojeruhiwa katika maandamano ya kudai Bobi Wine aachiwe huru.
Vurugu zilianza kutokea katika mji wa Kampala pamoja na miji mingine ya nchi hiyo Jumatano na tangu wakati huo vikosi vya usalama vimekuwa vikiwafyatulia risasi waandamanaji na kutmia vitoza machozi ili kudhibiti hali.
Akizungumza na wanahabari katika hospitali Kuu ya Mulago, Dr. Kaducu alisema hakuna aliyejuruhiwa anayestahili kulipa chochote kwasababu serikali imechukua jukumu la kugharamia matibabu.
“Gharama ya matibabu ni bure. Kama serikali, tunataka kusema, na liko wazi, hakuna raia atakayelipa pesa za matibabu wala hakuna atakayelipa pesa za matibabu ya upasuaji wowote. Serikali imechukua jukumu hilo,” Dr. Kaducu amesema.
Kulingana na gazeti la Nile Post, kuna wadi maalum iliyotengwa kwa ajili ya kushughulikia waliojeruhiwa katika jengo jipya la hospitali ya Mulago.
Bobi Wine alikamatwa Jumatano hatua iliyosababisha mauaji na majeruhi zaidi ya 60 huku wengine 321 kushikiliwa na polisi.
Bobi Wine anatarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo.
