
Waziri wa fedha wa Uingereza Rishi Sunak ametahadharisha hii leo kwamba uchumi wa taifa hilo unakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na janga la corona.
Waziri huyo ametoa matamshi hayo wakati serikali wiki ijayo ikitarajia kufanya mapitio ya matumizi yake.
Hata hivyo ameondoa uwezekano wa kurejeshwa kwa vizuizi vikali. Sunak amekiambia kituo cha utangazaji cha Uingereza cha Sky News kwamba utabiri wa kiuchumi unaotarajiwa kutolewa sambamba na mapitio hayo ya matumizi utaonyesha changamoto kubwa ya kiuchumi iliyopo sasa.
Licha ya athari kubwa ya virus vya corona kwenye mapitio hayo, lakini Sunak aliondoa kabisa uwezekano wa kurejeshwa kwa vizuizi vikali na tetesi zinazosambaa za kusitishwa kwa malipo kwenye sekta za umma.
Hii leo wizara ya fedha imetangaza kiasi cha dola bilioni 3 za kusaidia shirika la afya la nchini humo, NHS kukabiliana na athari za corona.