Afghanistan imedai kuzuia jaribio la mauaji ya Balozi wa Marekani mjini Kabul, lililopangwa kufanywa na kundi la kijihadi linalojiita Dola la Kiislamu IS, wakati wimbi la mauaji likiendelea kulikumba taifa hilo.
Maafisa wa ujasusi wa Afghanistan wameeleza kwenye taarifa yake kwamba wamefanikiwa kuvunja mtandao wa wanachama wanne wa IS katika jimbo la mashariki la Nangarhar, ambao walipanga kumuuwa mwanadiplomasia Ross Wilson, sambamba na maafisa wengine wa Afghanistan.
Wilson ambaye anakaimu ubalozi wa Marekani mjini Kabul tangu mwaka 2020, amelaani vikali mfululizo wa mashambulizi katika mji mkuu na miji mingine mikubwa, dhidi ya waandishi wa habari, wanaharakati na wanasiasa katika miezi ya hivi karibuni. Mashambulizi hayo yamesababisha hofu na ghasia licha ya kundi la Taliban na serikali kushiriki mazungumzo ya amani.
