Bahrain itafungua anga zake leo kuruhusu usafiri kati yake na Qatar. Mamlaka inayosimamia usafiri wa angani nchini humo imetangaza hayo jana Jumapili, kufuatia makubaliano ya wiki iliyopita yanayoungwa mkono na Marekani, ya kumaliza mzozo na Qatar.
Hatua hiyo imejiri baada ya Saudi Arabia kutangaza wiki iliyopita kwenye mkutano wa kilele kwamba imemaliza mzozo na Qatar.
Mzozo huo ulisababisha nchi nyingine za Kiarabu ikiwemo Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri kuvunja uhusiano wa kidiplomasia, kibiashara pamoja na usafiri kati yao na Qatar kuanzia katikati ya mwaka 2017.
Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, tayari zimetangaza kuruhusu usafiri wa ardhini, majini na angani kati yao na Qatar.
