Wapiga mbizi wa Indonesia watafuta kisanduku cheusi cha ndege


Wanajeshi wa majini nchini Indonesia wametoa video ya wapiga mbizi wakianza tena shughuli ya utafutaji mabaki ya ndege ya abiria iliyotumbukia baharini wikendi pamoja na kisanduku cheusi.

Ndege ya shirika la Sriwijaya Air aina ya Boeing 737 iliondoka uwanja wa ndege wa Jakarta ikiwa na watu 62, lakini ikapotea kwenye rada ikiwa inaelekea kisiwa cha Borneo Jumamosi.

Timu za uokozi tayari zimepata mabaki ya ndege pamoja na ya binadamu.

Maafisa husika tayari wamebaini eneo kilipo kisanduku cheusi cha mawasiliano cha ndege hiyo lakini bado hawajakipata.

Afisa mmoja amesisitiza umuhimu wa shughuli ya utafutaji ambayo imeanza tena kazi hiyo Jumatatu asubuhi, na kuitaja kuwa ni operesheni ya saa 24.

"Itakuwa ni operesheni isiyokuwa na ukomo," Rasman MS, mkuu wa shughuli hiyo ya utafutaji na uokozi amezungumza na wanahabari.

"Sasa hakutakuwa na mapumziko. Itakuwa bora tukipata waathirika kwa haraka."

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, baadhi ya wafanyakazi 2,600 sasa wako kwenye operesheni inayohusisha boti kadhaa na helikopta ambazo zinatumika kubeba miili, mabaki ya ndege na nguo za abiria ndani ya bahari kina cha takriban mita 23.

Pia kuna zaidi ya meli 50 pamoja na ndege zingine 13 zenye kuhusika na operesheni hiyo ya kutafuta mabaki ya ndege yenye usajili SJ182.

Mchunguzi wa Kamati ya Taifa ya usalama wa usafiri Indonesia amezungumza na shirika la habari la Reuters kwamba mamlaka ina matumaini ya kupata kisanduku cheusi cha mawasiliano Jumatatu.

Aliongeza kuwa kuna uwezekano ndege hiyo ilianguka na kukatika vipande vipande ilipogusa maji kwa kuzingatia mabaki yaliyopatikana.

"Kuna uwezekano ndege hiyo ilivunjika vipande vipande wakati inagusa maji kwasababu kama ingelipuka kwenye anga, vipande vyake vingekuwa vimesambaa sana," amesema urcahyo Utomo.

Wachunguzi tayari wanachunguza vifaa ambavyo vinaaminika kuwa gurudumu na sehemu ya kiwiliwili cha ndege.

Gurudumu kutoka moja ya injini pia ni miongoni mwa mabaki ambayo yamepatikana.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi