Wazazi wa wanafunzi wa darasa la saba wilayani Masasi watajwa kuwa chanzo kikuu cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu



Na Hamisi Nasri, Masasi 

   WAZAZI wa wanafunzi wa darasa la saba wilayani Masasi mkoani Mtwara wametajwa kuwa chanzo kikuu cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa elimu ya msingi wilayani humo kwa madai kuwa wazazi hao wamekuwa na tabia ya kuwashawishi watoto wao kujibu maswali vibaya ili wasifaulu mtihani wa taifa.

   Hayo yalisemwa jana wilayani Masasi na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Masasi,Changwa Mkwazu alipokuwa akijibu moja ya hoja kuhusu elimu na kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika shule zilizopo kwenye halmashauri hiyo,katika kikao cha Kamati ya ushauri ya wilaya ya Masasi (DCC) kilichoudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa na wazee maarufu na watendaji wa serikali.

  Alisema kuwa halmashauri ya wilaya ya Masasi ina jumla ya shule za msingi 126 na kwamba kumekuwa na hali ya kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika shule zake kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kupitia mitihani ya darasa ya saba. 

  Changwa alisema baada ya kushtushwa na hali hiyo inayojitokeza kila mwaka,halmashauri ilifanyika uchunguzi wa kina kwa lengo la kubaini chanzo na sababu inayopelekea kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba na kubaini kuwa wazazi wamekuwa na tabia ya kuwashawishi watoto wao siku ya kufanya mtihani wa taifa kujibu vibaya maswali ya kwenye chumba cha mtihani kwa madai ya kutokuwa na fedha za kuwasomesha. 

  Alisema katika uchunguzi huo walioufanya walizungumza na baadhi ya wanafunzi na kwamba baadhi wanafunzi walieleza kuwa wamekuwa wakikatazwa kufaulu mitihani yao hivyo siku ya kufanya mtihani wanatakiwa kujibu maswali vibaya kama walivyoagizwa na wazazi wao.

    “Wazazi wilayani Masasi bado wamekuwa na mwamko hasi katika elimu na kwamba wazazi wamekuwa mstari wa mbele kuwashawishi watoto wao siku ya mtihani wa taifa wa darasa la saba kujibu maswali vibaya ili wasifaulu …wazazi wanasema hali ngumu hawana fedha za kuwasomesha watoto wao iwapo wakifaulu,”alisema Mkwazu 

   Mkwazu alisema kutoka na hali hiyo halmashauri imejipanga kufanya uhamasishaji kwa kukutana na wazazi na walezi ili kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwekeza katika elimu kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwapatia haki ya kupata elimu watoto wao na kuondoa dhana potofu waliyonayo wazazi lakini halmashauri itaanya vikao maalumu vya ndani vya kujadili suala zima la elimu.

   Akisoma taarifa ya matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020 afisa elimu ya watu wazima, Ruth Tunzo kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya                 Masasi, Tunzo alisema kuwa waliofanya mtihani wa 2020 ni jumla ya wanafunzi 5836 sawa na asilimia 99.9 ambapo kati hayo wavulana ni 2697 na wasichana ni 3139 hata hivyo kumekuwa na kupungua kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi ukilinganisha na wanafunzi wanaanza elimu ya msngi.

   Alisema licha ya wazazi kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya mtihani wa kuhitimu elimu msingi lakini kumekuwa na sababu zingine ambazo pia zimechangia wanafunzi kufeli na kupelekea kushuka kwa ufaulu ikiwemo mimba za utotoni pamoja na utoro.


   “Kama kungekuwa na sheria ndogo ambazo zingekuwa zinawabana wazazi kuacha kuwatumia watoto ambao ni wanafunzi kufanya biashara ndogondogo kipindi cha shule kwenda na watoto kwenye ngoma za kigodoro ni wazi ingesaidia kumaliza hili tatizo la kushuka kwa ufaulu wilayani Masasi,”alisema Tunzo 

   Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Masasi Selemani Mzee alisema wazazi wanapaswa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao lakini pia serikali itaendelea kuhamasisha jamii juu ya mtoto kupata elimu.

   Alisema kuwa wazazi na walezi wenye watoto ambao wamefikia umri wa kwenda shule watoto wote wanapaswa kwenda shuleni ili waweze kupata elimu na kwamba mzazi ambaye hatampeleka mtoto wake shuleni serikali itamchukulia hatua kali za kisheria.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi