Spika wa bunge la Ghana jana amelazimika kuahirisha shughuli zake kwa muda wa wiki tatu kutokana na ongezeko la visa vya COVID-19 miongoni mwa wabunge na wafanyakazi.
Spika wa bunge Alban Bagbin, alitangaza kufungwa shughuli za bunge hadi Machi 20 kwa ajili ya kupunguza maambukizi.
Takribani wabunge 17 na wafanyakazi 151 wa bunge wameambukizwa virusi vya corona, ambavyo tayari viliingilia vikao vya bunge. Taifa hilo la afrika magharibi limesajili visa elfu 73,000 vya covid-19 na vifo vimefikia 482 huku watu 65,000 wakipona.
Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amepiga marufuku mikusanyiko mikubwa, harusi na hafla nyinginezo huku mipaka ikiendelea kudhibitiwa.
Mwezi uliopita rais huyo alionya kuwa kiwango cha maambukizi kinazidi kuongezeka na kinatishia kuathiri mfumo wa afya katika wimbi la pili la maambukizi.
