Kesi ya viongozi wa waasi wa Jamuhuri ya Afrika ya kati , iliyotarajiwa kuanza hii leo katika Mahakama ya Kimataifa (ICC) , imeahirishwa mpaka tarehe 16 mwezi Februari.
Alfred Yékatom na Patrice-Edouard Ngaïssona wanakabiliwa na makosa 21 na 32 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu Uhalifu unaodaiwa ni pamoja na kuongoza shambulio dhidi ya raia kwa makusudi.
Watashtakiwa kwa pamoja kwani mashtaka yanahusiana na mashambulio hayo hayo. Bw.Ngaïssona awali alikana mashtaka yote dhidi yake.
CAR ilitumbukia katika machafuko mwaka 2013 wakati waasi wengi wa Kiislamu kutoka kundi la Seleka walipochukua madaraka katika nchi yenye jamii kubwa ya Wakristo.
Kisha kundi lenye wanamgambo wengi wa Kikristo, lililoitwa anti-Balaka liliibuka ili kukabiliana na Seleka baada ya Rais François Bozizé kuondolewa madarakani.
Maelfu walipoteza maisha katika mapigano na Umoja wa Mataifa (UN) ulisema zaidi ya watu milioni moja walilazimika kukimbia makazi yao.
Bwana Ngaïssona alikuwa mratibu wa kisiasa aliyejitangaza mwenyewe wa vikosi vya anti-Balaka.
Katika jukumu hilo, ICC imesema alifanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwa ni pamoja na mauaji, kutesa na kuajiri watoto jeshini.
Kesi ya Bw Ngaïssona na Bw Yékatom itaanza wiki chache baada ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati kumkabidhi Mahamat Said Abdel Kani, kiongozi wa kikundi cha Seleka, kwa ICC kwa madai ya uhalifu uliofanywa katika mji mkuu, Bangui, mnamo 2013.
