Kutana na Baraka machinga asiyeona

 


Baraka Emmanuel (28) ni kijana mjasiriamali mwenye ulemavu wa macho (asiyeona).


Changamoto hii haijamkosesha fursa ya kujitafutia kipato, amekuwa anajishughulisha kufikia malengo aliyojiwekea.


Katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Arusha, Emmanuel alisema alizaliwa akiwa anaona vizuri, lakini mwaka 2000 akiwa na miaka saba alipatwa na tatizo la macho ambalo baada ya uchunguzi wa kina katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro aliambiwa ana presha ya macho.


Wazazi wake walimpeleka katika Shule ya Msingi Mchanganyiko yenye kitengo cha elimu maalumu Longido ambako alihitimu darasa la saba mwaka 2013, kisha akachaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Shinyanga alikohitimu kidato cha nne mwaka 2017.


Licha ya matokeo mazuri ya mitihani ya kidato cha nne, ambapo alipata daraja la pili, aliamua kutoendelea na masomo ya kidato cha tano na sita ili aanze shughuli za ujasiriamali zitakazomwezesha kujikimu na kumsaidia mama yake mzazi.


“Nilikuwa napata fedha nyingine natumia na zinazosalia naweka akiba ili nizitumie kulipia ada ya kujifunza utayarishaji wa muziki,” alisema Emmanuel.


Alisema ratiba yake ya kutwa hutegemea na namna alivyofanya biashara kwa siku iliyotangulia ikiwamo eneo atakaloanzia shughuli zake.


“Ninaishi sehemu inaitwa Habari Maalumu mbele ya Ngaramtoni wilaya ya Arumeru (umbali wa takribani kilometa 12 kutoka katikati ya jiji la Arusha) kuna siku napanda daladala hadi Ngaramtoni nashuka naanza kutafuta wateja hadi nafika mjini, huwa nabadilisha mbinu za kuwafikia wateja wangu,” alisema Emmanuel.


Alisema katika kipindi ambacho amekuwa akiuza viberiti amekuwa anapata wateja na kipato ambacho si kikubwa kwa sababu ya aina ya bidhaa.


“Unajua bidhaa ninazoziusa si zile zinazotumika sana, ndiyo maana napata kipato kidogo pia, japo kinanisaidia na kuepukana na tabia ya kuombaomba kama wanavyofanya wengine wenye ulemavu kama mimi,” alisema.


Emmanuel alisema kuna watu akikutana nao kwa mara ya kwanza huwa hawaamini kama yeye haoni, hudhani anaigiza kwa sababu macho yake hayaonyeshi kuwa na tatizo kama wengine wenye ulemavu wa aina hiyo.


“Nikikuelekezea macho yangu utadhani naona kwa sababu lensi hazikuathirika kabisa bali mishipa ya macho ndio ilipata athari na kusababisha ugonjwa unaoitwa presha ya macho, kwa hiyo sioni kabisa natumia hii fimbo ya watu wenye ulemavu wa macho kunisaidia kutambua njia,” alisema Emmanuel.


Kutokana na hali yake alisema anatambua fedha za noti kwa kuzigusagusa kwa kutumia alama maalumu za kuzitofautisha kati ya moja na nyingine kulingana na urefu wake pamoja na upana hivyo kuwarudishia wateja chenji bila kukosea.


Alisema wateja wake pia wamekuwa wakimpa ushirikiano anapokuwa anawarudishia chenji au kuchukua fedha baada ya kuwapa bidhaa kwa kuona namna alivyoamua kujishughulisha badala ya kuwa ombaomba.


Kuhusu namna anavyoweza kutumia fimbo yake kumwongoza anasema sio watu wengi wanaofahamu maana ya fimbo za walemavu wa macho hasa madereva wa vyombo vya moto jambo ambalo ni changamoto kwa usalama wake.


“Wakati mwingine madereva wa daladala au gari lolote wananisukuma wakidhani nafanya makusudi kuingia barabarani kwa sababu tu wananiona nikifanya umachinga wakifikiri naona kumbe nina ulemavu wa macho sioni kabisa,” alisema na kongeza:


“Jamii hasa madereva waone umuhimu wa kuwasidia wenye ulemavu ili wasigongwe na magari,” alisema.


Alisema kabla ya kufanya ujasirimali jijini Arusha alishafanya shughuli hizohizo jijini Dar es Salaam karibu masoko yote akiuza viberiti ikiwa ni njia ya kujikwamua kiuchumi.


Aliyataja maeneo ambayo amewahi kufanya biashara hiyo kuwa ni Kariakoo, Tandamti, Lumumba na Gerezani.


Alisema hata katika maandiko matakatifu mwenyezi Mungu anasisitiza watu kufanya kazi ili kupata chakula au kipato, hivyo watu wenye ulemavu hawapaswi kutumia hali zao kama chanzo cha mapato au kusubiri kupewa kila kitu na watu walio karibu nao bali watumie hali zao kufanya kazi zinazoenda na mazingira waliyonayo.


Mjasirimali huyo alisema kutokana na maisha yake kutishiwa na vyombo vya moto hasa magari na pikipiki wasioelewa fimbo ya watu wenye ulemavu wa macho anaomba wasamaria wema wanaoweza kumwezesha kuwa na duka atakalokaa sehemu moja kuhudumia wateja wake.


Alisema pamoja na biashara hiyo kuzalisha kipato kidogo, anachokipata kinamsaidia kupata mahitaji yake binafsi, mama yake pamoja na mdogo wake anayesoma elimu ya ufundi mkoani Kilimanjaro na kulipa pango la mwezi katika nyumba wanayoishi.


Daktari wa macho azungumza

Mtaalamu wa tiba za macho kutoka Msimbazi Eye Center jijini Arusha, Dk Alina Nasser alisema kitaalamu ugonjwa wa presha ya macho unaitwa “Glaucoma” ambao chanzo chake kinaweza kuwa cha kurithi katika familia.


Alisema sababu ya pili inayoweza ni kuumizwa sehemu ya macho na kitu chochote na ukigundulika mapema unatibika, ukichelewa unaua haraka mishipa ya macho.


“Mshipa wa macho ukiathirika hauna matibabu ya kufanya macho yaone tena hali ya uono au kuona kunapungua, zipo dawa za kudhibiti mishipa ya macho isiendelee kuathirika zaidi pia kuna uwezekano wa kufanyika upasuaji,” alisema Dk Alina


Mfanyabiashara wa matunda Soko la Arusha, Angella Kimaro anasema alianza kumwona Emmanuel tangu mwaka 2019 akiuza viberiti na kuwa mmoja wa wateja wake hadi sasa .


“Ni kijana anayependa kujishughulisha licha ya ulemavu wake wa kutokuona lakini aliona asikae nyumbani au kuomba omba kando kando ya barabara.


Alisema watu wanamfahamu na kutokana na hali yake watu wamekuwa wepesi kununua viberi kutoka kwake,” alisema Angella.


Alisema watu wenye ulemavu unaofanana na Emmanuel hawapaswi kuona dunia imefika mwisho watumie fursa zilizopo kujitafutia kipato, msaada utawakuta wakijendeleza badala ya kuwa tegemezi kwa asilimia 100.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi