Mahakama ya Mwanzo Buguruni imevunja ndoa iliyodumu kwa miaka saba kati ya Janeth Madege (33) na Caristus Luoga (34) kutokana na madai ya mume kukosa uaminifu.
Janeth ambaye alifunga ndoa ya Kikristo mwaka 2013, alifungua kesi ya kudai talaka, machumo ya pamoja na matunzo ya mtoto kutoka kwa mumewe Luoga kwa madai hakuwa mwaminifu.
Hakimu Mkazi, Mwinyiheri Kondo alifikia uamuzi wa kuvunja ndoa hiyo baada ya kuridhika kuwa ushahidi uliotolewa na Janeth ambao haukuwa na shaka. Hadi ndoa hiyo inavunjwa, Janeth na Luoga walikuwa wamejaliwa kupata mtoto mmoja.
Janethm mkazi wa Kinindoni alimtuhumu mumewe kwa kuishi na mwanamke mwingine.
Alidai matatizo katika ndoa yao yalianza mwaka 2016 aliposafiri kwenda Muscat nchini Oman kwa ajili ya kununua bidhaa za kuuza. Alidai aliporudi nyumbani kwao eneo la Goba, Dar es Salaam alimkuta mumewe akiwa na mwanamke mwingine ndani ya nyumba yao.
Janeth alisema alipohoji mumewe alimpiga na kumwambia aondoke, hivyo alilazimika kwenda kuishi nyumbani kwa wazazi wake. Alisema hata alipokuwa akifuatilia matumizi ya mtoto, mumewe alikuwa akimfukuza na kumnyama fedha za matunzo ya mtoto.
Akijitetea, Luoga aliieleza mahakama kuwa mkewe aliondoka nchini kwenda Oman, aliporudi alikwenda moja kwa moja kuishi nyumbani kwa wazazi wake.
Alidai aliamua kutafuta mwanamke mwingine wa kuishi naye baada ya kuona mkewe amefikia kwa wazazi wake na jitihada za kutaka arudi zilishindikana.
Mwanaume huyo alikubali kugawana mali walizochuma wote na aliomba mahakama iruhusu mtoto abaki kwake ili amlee.
Ndoa yavunjwa
Akisoma uamuzi wake, Hakimu Kondo alitumia kifungu cha 107 (2) cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoiruhusu mahakama kutoa hati ya talaka endapo itathibitisha mdaiwa anajihusisha na uasherati.
“Kuanzia leo (Jumatatu) Janeth na Luoga si wanandoa, hivyo mahakama hii inaamuru wagawane nyumba iliyopo eneo la Goba kwa thamani sawa na kwamba samani zote zilizomo ndani ya nyumba hiyo ni mali ya Janeth,” alisema hakimu huyo.
Pia aliamuru mtoto waliyezaa abaki kwa mama yake na kwamba baba anapaswa kupeleka fedha fedha za matumizi Sh50,000 kila mwezi na huduma ya matibabu kadiri inavyotakiwa.
Hakimu Kondo alisema Luoga ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 45 endapo hajaridhika na hukumu hiyo.
