Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.
Mashindano ya kitaifa ya kutafuta wabunifu wa teknolojia MAKISATU yanatarajiwa kuanza mwezi March mwaka huu yakishirikisha wabunifu wa teknolojia kutoka makundi mbalimbali , mashindano yatakayokwenda sambamba na maonyesho mbalimbali ya bunifu zilizobuniwa hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Feb. 5, 2021 jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Taknolojia Dkt Leonard Akwilapo amesema mashindano hayo kwa mwaka 2021 yataanza march 20 hadi 26 ambapo wabunifu mbalimbali wa hapa nchini wataonyesha bunifu zao zitakazoweza kusaidia katika Maendeleo ya nchi.
" Mashindano haya yamekuwa yakifanyika huu mwaka wa tatu sasa niombe watanzania wote wenye bunifu waweze kujitokeza kuonyesha bunifu walizobuni ili ziweze kuendelezwa na kuleta tija kwa taifa" amesema Dkt Akwilapo.
Amesema mpaka sasa ikiwa ni mwaka wa tatu mpaka sasa kuna bunifu elfu moja na sitini na sita 1066 wametambuliwa na kati ya hizo bunifu 130 zimeendelezwa na zipo katika hatua za mwisho kuanza kutumika katika kurahisisha kazi.
Aidha amebainisha kuwa katika kuimarisha uratibu wa bunifu hadi ngazi ya chini wameanza kuimarisha uratibu wa tafiti hadi katika Serikali za mitaa itakayoweza kuratibu hadi ngazi ya vitongoji kuwaibua wabunifu walionje ya mfumo.
Ametaja makundi yatakayoshiriki mwaka huu ni " shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya ufundi VETA, Vyuo vikuu, taasisi za utafiti na kundi lililo nje ya mfumo yani mfumo usio rasmi" amesema.
Aidha amesema usajili ulianza tangu novemba 18, na inatarajiwa kufungwa Feb.15, 2021, na kundi la Vyuo vikuu na taasisi za utafiti vitaratibiwa na COSTECH, Vyuo vya ufundi stadi na wa mfumo usio rasmi vitaratibiwa na VETA, na Shule za Msingi na Sekondari zitaratibiwa na TAMISEMI, na vyuo vya ufundi vitaratibiwa na NACTE.
Aidha amesema ifike wakati viwanda vya ndani ya nchi kuanza kutumia teknolojia zilizobuniwa hapa nchini ikiwa ni zile zinazotokana au zinazoibuliwa kupitia mashindano ya MAKISATU.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Dkt Amos Nungu amesema wamekuwa wakiwaratibu wabunifu wote na wabunifu wengi husaidiwa kwa kuunganishwa na taasisi zinazohusika ili kuwaendeleza.
" Mfano wa kule kusini mbunifu wa helkopta alisaidiwa kwa kuunganishwa na vyuo vinavyohusika na ubunifu wake, wengine anaunda kitu lakini unashindwa kuelezea kiundani lakini akipelekwa kwenye kumbi maalumu za wabunifu kule anaweza kusaidiwa na kusaidia wengine" amesema Dkt Nungu.
Mashindano ya MAKISATU kwa mwaka huu yataongozwa na kauli mbiu isemayo "Sayansi, Taknolojia na ubunifu kwa uchumi endelevu"
