Waziri wa mambo ya nje wa Qatar amesema nchi yake iko tayari kusaidia katika hatua za kuuimarisha uchumi wa Lebanon unaoporomoka.
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema Qatar itasaidia ikiwa tu wanasiasa wanaovutana nchini humo watakubaliana kuhusu serikali mpya.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Qatar aliyekwenda Lebanon amezungumza na waandishi wa habari na kutowa ahadi hiyo baada ya kuwa na mkutano na rais wa Lebanon.
Al Thani amesema sera ya nchi yake inaweza tu kuruhusu utoaji wa msaada wa kifedha kupitia miradi ya kiuchumi ambayo itahitaji usimamizi wa serikali huru itakayofanya kazi na Qatar.
Lebanon iko katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi ambao haujawahi kutokea kwa miongo na inahitaji kwa dharura msaada wa kimataifa lakini nchi wahisani zimetowa masharti ya kuitaka iwe na baraza huru la mawaziri litakalokuwa tayari kufanya mageuzi.