Sakata la kuibuka kwa ugonjwa wa ajabu katika kata ya Ifumbo wilaya ya Chunya mkoani hapa kwa wananchi kutapika damu na kupoteza maisha limeingia sura mpya huku baadhi ya wananchi wakitilia shaka matumizi ya maji yasiyo salama kutokana na baadhi ya vijiji kuwa na changamoto hiyo.
Sakata hilo liliibuka Februari 6, mwaka huu kwenye kikao cha baraza la madiwani wilaya ya Chunya baada ya Diwani wa Kata hiyo, Weston Mpyila kueleza kuwepo kwa ugonjwa huo na hatua ambazo zimechukulia na halmashauri.
Iliripotiwa kuwa kulikuwa na vifo vya watu 15 na wengine 50 kuugua jambo lililozua sintofahamu ya ugonjwa huo.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Diwani wa Kata ya Ifumbo, Weston Mpyila alisema kuwa kufuatia kuripotiwa kwa ugonjwa huo katika mitandao ya kijamii, televisheni na magazeti, Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila amefika kutembelea kata hiyo akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na kuzungumza na wananchi.
Alisema ujio wa Chalamila umeleta matumaini mapya kwa wananchi baada ya kuahidi kushughulikia maombi yao ya ujenzi wa kituo cha afya na miundombinu ya barabara ambazo ni changamoto zilizochangia watu huko kukosa matibabu.
Alisema mbali na serikali kutekeleza maombi hayo ya wananchi na kutuma wataalamu kwenda kuchunguza tatizo la ugonjwa huo pia wanatilia mashaka maji yanayotumiwa na wananchi huenda ikawa chanzo kwani wilaya hiyo ina changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama na kuna wakati wanategemea maji ya visima na mvua kwa matumizi ya kunywa na kupikia.
"Chunya kuna changamoto kubwa ya tatizo la maji licha ya kata Ifumbo kuunganishiwa maji katika wilaya ya Mbeya Vijijini lakini inapotokea shida ya uhaba wa maji wanalazimika kutumia ya visima ambayo kwa matumizi ya nyumbani sio salama hivyo kusababisha magonjwa ya homa za matumbo lakini kwa sasa tunasubiri watalaamu waje wachunguze tatizo la kuibuka ugonjwa wa kutapika damu," alieleza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Chalamila, akiwa na kamati ya ulinzi na usalama walitembelea kata hiyo leo Februari 7,2021, sambamba na kuzungumza na wananchi ambao walimuomba kuboreshewa miundombinu ya barabara, kituo cha afya ili wanapougua waweze kupata huduma mapema na kuokoa maisha yao .
Chalamila ametuma timu ya wataalamu kwenda kuchunguza sababu za kuibuka kwa ugonjwa na kuagiza wagonjwa waliopo wachukuliwe sampuli zao ili zikapimwe na kujua chanzo chake huku wakiendelea na matibabu .
Pia ameagiza wagonjwa waliopo kuhamishiwa kwenye hosptali hususani ya rufaa kanda ili waendelee na matibabu wakati serikali ikisubiri majibu ya timu ya wataalamu waliokwenda kuchunguza suala hilo.
