Muungano wa vyama vya upinzani nchini Somalia umependekeza kuundwa kwa Baraza la Taifa la wabunge, viongozi wa upinzani na mashirika ya kiraia kuongoza taifa hilo la Pembe ya Afrika baada ya muda wa rais kumalizika leo bila kuwepo na mpango wa kukabidhi madaraka.
Muungano huo wa upinzani umesema utakataa jaribio lolote la kuongezea muhula wa rais Mohamed Abdullahi Mohamed, na umependekeza kwamba baraza linaweza kuchagua kiongozi wa mpito hadi rais mpya atakapochaguliwa na wabunge.
Hakukuwa na tamko kutoka ofisi ya rais, lakini wasaidizi wake walikuwa wanatoa pendekezo la kurefusha muhula wake. Katika taarifa iliyotolewa na ubalozi wake mjini Mogadishu, Marekani ilimuhimiza Mohamed kuchukua hatua sasa hivi kutatua mkwamo wa kisiasa, na kutafuta makubaliano na viongozi wa majimbo ya shirikisho ili kufanya uchaguzi wa bunge na rais mara moja.
