Maafisa wanasema Bunge la Ulaya limeidhinisha mkataba wa maelewano ya kibiashara wa Brexit lakini limeionya Uingereza kutimiza ahadi zake.
Wabunge 660 wameunga mkono makubaliano hayo ya kibishara huku watano wakipinga na wabunge 32 hawakuhudhuria kikao hicho cha upigaji kura.
Makubaliano hayo yanaweka wazi mkakati wa uhusiano mpya kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, miaka mitano baada ya Waingereza kupigia kura kujiondoa kutoka kwenye umoja huo baada ya kuwa mwanachama kwa miaka 47.
Waziri wa Uingereza wa Brexit David Frost ameipongeza hatua hiyo ya makubaliano aliyosaidia kuyafikia baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa miezi kadhaa akiwa pamoja na mwenzake wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier.
Kura hiyo inautilia kikomo mchakato wa miaka mitano wa Brexit ambao uliigawa vibaya Uingereza na kusababisha amani ya kisiwa cha Ireland kutiliwa mashaka.
