SERIKALI imetenga Dola za Kimarekani milioni 120 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Bonde la Mto Msimbazi,” ameeleza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Hamad Hassan Chande.
Chande ameyasema hayo leo Bungeni Dodoma wakati akijibu Swali la Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mto Msimbazi ambao umeainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025.
Katika majibu yake, Naibu Waziri amesema kuwa Serikali kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DFID) imetenga Dola za Kimarekani milioni 20.
Amesema pia Benki ya Dunia, kupitia Mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (DMDP), imekubali kutoa mkopo wa nyongeza wa Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Bonde la Mto Msimbazi.
Aidha amesema kuwa Serikali imepanga kulibadili eneo la bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji na fursa mbalimbali.
“Ili kufikia azma hiyo, usanifu wa mradi huo umekamilika. Utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kupata idhini ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo za mkopo kupitia Wizara ya Fedha na Mipango,” amesema Chande.
Aliongeza kuwa ili kupunguza athari za mafuriko kwa sasa, kipande cha Mto Msimbazi cha daraja la Jangwani kinafanyiwa usafi wa mara kwa mara na wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mradi huo ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) yenye lengo la kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project - DMDP) kwa mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia.
Aidha, Serikali kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DFID), inatekeleza program ya “Tanzania Urban Resilience Programme (TURP)” ambayo imelenga kuzisaidia Halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
