Huyu ndiye Dk Blandina Kilama, msaidizi wa uchumi wa Rais Samia

 


Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan jana Ijumaa Aprili 16, 2021 alifanya uteuzi wa wasaidizi wake wanane katika ofisi binafsi ya rais Ikulu watakaokuwa wakimshauri na kumsaidia mambo mbalimbali katika kazi zake.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Gerson Msigwa miongoni mwa wateule hao ni Dk Blandina Kilama ambaye sasa ni msaidizi wa uchumi wa Rais Samia.


Katika nafasi hiyo Dk Kilama atakuwa anawajibika kumshauri kiongozi mkuu huyo wa nchi katika mambo yote yanayohusu  uchumi.


Dk Blandina ni mchumi aliyebobea pia katika utafiti, mafunzo na uchambuzi wa sera, akiwa mtafiti mwandamizi ushiriki wake kupitia mazungumzo na machapisho ya ndani na nje kuhusu masuala ya uchumi yameleta mapinduzi chanya kwa kuwainua wanawake na kupunguza umasikini.


Kwa sasa anafanya utafiti na Taasisi ya Repoa kuhusu takwimu na utengenezaji wa sera na ushirikishaji wa umma na huko nyuma amewahi kufanya tafiti mbalimbali kuhusu umasikini na maendeleo ya watu na nyingine nyingi kuhusu mnyororo wa thamani katika kilimo na maendeleo.


Mwaka 1998 hadi 2001,  Dk Kilama alisoma shahada yake ya kwanza ya uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwaka 2001 hadi 2003 alisoma shahada ya pili ya utawala wa umma katika maendeleo ya kimataifa Chuo kikuu cha Harvad ..


2007 hadi 2013,  Dk Blandina alisoma shahada ya uzamivu katika chuo Kikuu cha Leiden nchini Uholanzi na utafiti wake ulikuwa katika sekta ya korosho nchini Tanzania akilinganisha na Vietnam akionyesha kwa namna gani kilimo kinaweza kumaliza umasikini.

Post a Comment

0 Comments