Taasisi za Umma na Binafsi zatakiwa kuweka mfumo wa utawala na usalama


Na Thabit Madai, Zanzibar.

TAASISI za Umma na Binafsi zimetakiwa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanaweka mifumo mizuri ya utawala, Usalama na afya  kazini ili kuwakinga wafanyakazi na ajali pamoja na maradhi katika maeneo yao ya kazi

Aidha Taasisi hizo zimetakiwa kutenga rasilimali za kutosha katika mipango kazi yao ya kila siku  kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi na majanga yanayoweza kuwatokea wakati wa kazi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi,Afisi ya Rais Kazi,Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga wakati akitoa taarifa maaluum kwa Waandishi wa Habari juu ya  Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Usalama na Afya kazini, ambapo taarifa hiyo imetolewa Wizarani hapo Mwanakwerekwe Mjini Unguja.

Soraga alisema, Taasisi zote za kazi ziwe za Umma au  binafsi, kushirikiana na Serikali zinatakiwa kuweka mifumo mizuri ya utawala ya Usalama na afya kazini kama ilivyobainishwa katika mkataba wa Usalama na Afya Kazini wa mwaka 2006 namba 187.

“Pia tuweke rasilimali za kutosha katika mipango kazi yetu ili kukinga ajali na maradhi kwenye maeneo yetu ya kazi kwa kuzigatia kuwa pato kubwa la nchi linatokana na wafanya kazi wenye afya njema na walio katika mazingira bora ya kazi,”alisema

Aliongeza kuwa, Taasisi hizo zinatakiwa kuwashirikisha wafanya kazi wenyewe katika kufanya tathimini ya hatari zinazowakabili katika kazi zao.

Katika hatua nyingine Waziri Soraga alitoa wito kwa taasisi hizo kuhakikisha zinawalinda wafanya kazi katika sekta mbalimbali za kiuchumi  na hatari za kiusalama ikiwemo maambukizi ya virusi vya Corona (Covid 19).

“Ni muhimu sana kuwalinda wafanyakazi wetu kwa ustawi wa maisha yao, familia zao na Nchi kwa ujumla kiuchumi na hata kijamii ikiwemo kufikia lengo lililokusudiwa kujenga uchumi wa Buluu wenye nguvu,” alibainisha.

Waziri Soraga akizungumzia maadhimisho hayo kwa mwaka huu alisema kuwa Zanzibar kupitia Wizara yake inaungana na jamii ya kimataifa kuadhimisha siku siku ya kimataifa ya Usalama na Afya kazini ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Aprili 28.

Alisema, katika kuadhimisha siku hiyo Zanzibar pia inahakikisha kuwa inasimama imara katika kukabiliana na  athari za Virusi vya Corona kwenye maeneo ya kazi kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na waataalamu wa afya.

“Afisi ya Rais,Kazi,Uchumi na uwekezaji itaendelea kushirikiana na kushirikiana na vyama huru vya wafanya kazi(ZATUC), Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA) na taasisi nyingine za ndani na Nje ya Nchi kuhakikisha kuwa tunaweka mikakati ya kuimarisha mifumo ya kitaifa ya Usalama na afya kazini ili kukabiliana na athari itokanazo na virusi vya Corona (COVID - 19) na maradhi mengine yanayojitokeza maeneo ya kazi,” alieleza Soraga.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Kazini huazimishwa kila mwaka ambapo kauli mbui ya mwaka huu inasema,’Tarajia,jitayarishe na kukabiliana na matatizo yoyote yasiyokuwa ya kawaida- Wekeza sasa kwenye mifumo inayohimili vyema masuala ya Usalama na Afya Kazini’.

 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi