Walimu wilayani Kilolo wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kujihususha kimapenzi na wanafunzi kwani kufanya hivyo ni kukiuka maadili, kudhalilisha kazi ya ualimu, kuhatarisha ajira na kukatisha ndoto za wanafunzi.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape alipofanya mkutano na walimu wa Wilaya hiyo kwa lengo la kutoa elimu juu ya sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa walimu.
Katika Mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilolo iliyopo wilayani hapo, Hape alieleza kuwa Kilolo ni moja ya Wilaya zenye idadi kubwa ya mashauri ya nidhamu yanayohusu walimu kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanafunzi, jambo ambalo linadhalilisha kazi ya ualimu.
“Kilolo kuna tatizo kubwa la walimu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi, wote tunatambua kuwa hii ni kuvunja miiko na maadili ya ualimu. Wazazi wametukabidhi watoto ili tuwalee kimwili, kiroho na kiakili lakini baadhi yetu wamewafanya wanafunzi kuwa wapenzi wao, jambo hili halivumiliki,” alisema Hape.
