Israeli imefanya mashambulizi kadhaa alfajiri ya leo katika Ukanda wa Gaza, baada ya wanamgambo wa Palestina kurusha makombora ya roketi katika miji iliyopo kusini mwa Israeli.
Mashambulizi ya alfajiri ya Jumatatu ni makubwa zaidi tangu mapambano yaanze wiki moja iliyopita.
Israeli inasema imeshambulia majengo yanayomilikiwa na wanamgambo wa Hamas pamoja na nyumba kadhaa za makamanda wa kundi hilo, hata hivyo barabara kuu kadhaa na nyaya za umeme pia zimeharibiwa.
Mashambulio hayo yanatokea wakati jumuiya ya kimataifa ikitaka pande zote mbili katika mgogoro huo kusitisha mashambulizi.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) lilifanya mkutano wa dharura jana Jumapili na Katibu Mkuu wa UN António Guterres ameonya kuwa mapambano zaidi "yanaweza kusababisha hali mbaya ya kiusalama na kibinaadamu."
Guterres pia ametaka mapambano hayo "mabaya" yasitishe haraka iwezekanavyo.
Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi ameeleza leo Jumatatu kuwa nchi yake "imepiga hatua kubwa katika kutafuta kusitishwa kwa mapambano...na matumaini bado yapo."
Lakini mpaka sasa hakuna dalili za hilo kutokea huku mapambano makali yakiingia wiki ya pili.
Ghasia hizo ni zao la wiki za hamaki na wasiwasi baina ya Israeli na Palestina katika eneo la Jerusalemu Mashariki ambapo hali hiyo iliishia katika mapambano katika eneo takatifu kwa Waislamu na Wayahudi.
Kundi la Hamas, ambalo linaongoza Ukanda wa Gaza, likaanza kurusha makombora ya roketi baada ya kuionya Israeli iondoke katika eneo hilo la Jerusalemu, na hapo ndipo Israeli ilipoanza kufanya mashambulizi ya anga ya kulipiza.
