Njombe:Wafanyabiashara wataka wasio kwenye maeneo rasmi waondolewe kunusuru soko kuu


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wafanyabiashara mjini Njombe wameiomba serikali kuwahamisha wafanyabiashara wanaofanya biashara zao maeneo yasiyo rasmi ili kulinusuru soko kuu jipya ambalo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni kumi.

Ombi hilo wamelitoa kwenye kikao kilichokutanisha wafanyabiashara wa mkoa wa Njombe, mamlaka ya mapato Tanzania (TRA)  mkoa wa Njombe chini ya mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya.

Walisema bidhaa nyingi zinazopatikana ndani ya soko kuu nje zimetapakaa kila sehemu hivyo kuwaathiri wanaofanya biashara ndani ya soko hilo kwa kuwa wanalipa ushuru wakati wanaofanya biashara nje ya soko hilo hawalipi chochote. 

Walisema kutokana na hilo biashara ndani ya soko inashindwa kufanyika kwa kukosa wateja huku mwisho wa mwezi ukifika wanashindwa kulipa hata kodi za meza.

Baadhi ya wafanyabiashara  hao wakiwemo Joseph Mapunda na Dancan Kyando walisema changamoto wanayoipata ni kushindwa kuuza bidhaa zao kwa kuwa wapo wanaotembeza bidhaa mitaa hivyo wateja kushindwa kufika katika soko hilo.

"Baadhi ya wafanyabiashara wanauza bidhaa zao kando ya barabara na wengine wanatembeza mitaani hivyo wateja wanashindwa kuja katika soko hili hivyo tunashindwa kuuza" alisema Malinda. 

Mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya alisema ameelekeza kuwa pamoja na kuwaondoa wafanyabiashara maeneo yasiyo rasmi lakini gari ziwe zinashusha na kupakia abiria ili kuvutia wateja kwenda kwenye soko hilo.

Alisema serikali imetoa kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya bilioni kumi ili kulijenga soko hilo la kisasa lakini limekuwa likitumika kwa kiwango kisichoridhisha.

"Ni kweli zipo changamoto ambazo ni muhimu tukazifanyia kazi lakini tunachokisema wapo wafanyabiashara katika soko hili wana vizimba lakini wanawatuma vijana wao kuuza bidhaa nje ya soko hilo halikubaliki" alisema Rubirya.

"Haiwezekani tujengewe soko la bilioni kumi halafu tukafanya biashara barabarani kulikuwa na haja gani serikali kuandaa fedha zote hizo? " alisema Rubirya. 

Alisema serikali imeandaa mpango mzuri ambao utahakikisha wafanyabiashara wote wanaingia kwenye soko jipya na watakaokosa nafasi watapelekwa kwenye maeneo mengine ya masoko ikiwemo la Joshoni na lile la machinjioni. 

Kaimu meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania mkoa wa Njombe Zabron Walwa aliwataka wafanyabiahara kwenye soko hilo ambao wana malalamiko  kufika katika ofisi za TRA mkoa wa Njombe ili kuweza kutatuliwa.

"Wafanyabiashara wa soko kuu wanaolalamika kushindwa kulipa kodi kutokana na kutofanya biashara wafike ofisini kwetu na tuone namna ya kufanya" alisema Zabron. 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi