Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limesema leo kuwa, limewaokoa zaidi ya watu 150 waliokuwa wameshikiliwa mateka na kundi la waasi la ADF, linalolaumiwa kufanya mauaji ya maelfu ya watu mashariki mwa nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi katika mkoa wa Ituri Jules Ngongo, amesema jeshi limefanikiwa kuwaokoa zaidi ya watu 150 wengi wao wakiwa wanawake, wazee na watoto.
Ngongo amesema hilo limewezekana kufuatia oparesheni ya kijeshi dhidi ya waasi wa ADF iliyofanyika kuanzia Julai 18 hadi 20 katika maeneo ya Boga, Tchabi na Irumu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Mwishoni mwa mwezi Mei, mamlaka nchini humo iliwashtumu waasi wa ADF kwa kuua raia wasiopungua 50 katika maeneo ya Boga na Tchabi, pamoja na kushambulia kambi ya wakimbizi iliyoko Irumu.
