Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ ametoa wito kwa Watanzania kuwa na imani na Serikali kuhusiana na utoaji chanjo ya ugonjwa wa corona.
Mzee wa Upako ametoa rai
hiyo leo Jumatano Julai, 28, 2021 katika hafla ya uzinduzi wa chanjo ya
covid–19 iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema ili
kupambana na janga hilo lililokumba ulimwengu mzima ni lazima nchi iwe
na umoja na kushirikiana kwa pamoja kwani Serikali imejiridhisha vya
kutosha juu ya chanjo hiyo.
“Wote tunakubali kwamba corona ni
vita na hatuwezi kuishinda kama hatuna umoja, tuna Wizara ya Afya,
Waziri Mkuu yupo sidhani kama hawa wenzetu wanaweza kuitoa nchi kafara
kwamba watu wapate chanjo halafu wafe, lazima mifumo ya nchi yetu
imejiridhisha, haitakuwa 100 kwa 100 kila kitu kina mapungufu lakini
tujenge imani,”
“Mimi ni muhubiri wa zamani nilianza kuhubiri
injili wakati wa Kambarage niwaombe maaskofu wenzangu tujenge imani kwa
Serikali yetu na Wizara ya Afya, tunachanja kwa nia njema kwa ajili ya
afya zetu, watakaosema Mzee wa Upako anajipendekeza sawa tu kwani
akutukanaye hakuchagulii tusi,” amesema.
Ameongeza kuwa watu
walimnukuu vibaya Hayati Dk John Magufuli kwani hakusema watu wasichukue
chanjo bali umakini uwepo na kwamba tayari wameshajiridhisha kuwa nchi
itakuwa salama
“Uzuri Tanzania ni nchi ya ajabu katika Bara la Afrika hivyo tusiogope wala kufadhaika kwani tunafanya haya kwa nia njema,” amesema Mzee wa Upako.
