Mkuu mpya wa jeshi la Afghanistan chini ya utawala wa Taliban Qari Fasihuddin ameapa leo kuwasambaratisha wapinzani wa kiafghani watakaoiteteresha nchi hiyo kupitia njia za uasi, madai ya haki kwa makundi ya kikabila na demokrasia.
Matamshi ya kamanda huyo wa ngazi ya
juu aliyoyatoa kwenye kongamano moja mjini Kabul yamenukuliwa na vyombo
kadhaa vya habari nchini Afghanistan pamoja na mitandao ya habari yenye
mafungamano na Taliban.
Fasihuddin anayefahamika pia miongoni mwa
wapiganaji wa Taliban kama "mbabe wa kaskazini" amesema wapinzani
wanalenga kuvuruga usalama na kuitumbukiza Afghanistan kwenye vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
Mkuu huyo wa jeshi pia amearifu kwamba Afghanistan
iko mbioni kuunda jeshi imara litakalokuwa na uwezo wa kuilinda nchi
hiyo baada ya kusambaratika kwa jeshi la serikali iliyoangushwa.
