Na Ahmad Mmow, Lindi.
Wakala wa barabara za mijini na vijijini ( TARURA ) manispaa ya Lindi imepanga kuzifanyia matengenezo barabara ambazo hazipitiki wakati wote.
Hayo yalielezwa jana mjini Lindi na meneja wa TARURA wa manispaa ya Lindi, Wahabu Nyamzungu alipozungumza na waandishi wa habari ili kueleza mipango ya TARURA kuzifanyia matengenezo barabara zisizopitika wakati wote.
Mhandisi Wahabu alisema wakala huo umedhamira kufungua barabara nyingi hambazo hazipitiki wakati wote na kufanya matengenezo maeneo korofi.
Mhandisi Wahabu ambae ni kaimu mratibu wa TARURA wa mkoa wa Lindi alibainisha kwamba kwa sasa wameanza na barabara ya Nangaru-Chikonji. Ambapo wataanza kujenga barabara ya Mtange-Kibaoni.
" Kwakuanzia, mwaka huu tutaanza na Mtange kwenda Kibaoni, Kibaoni hadi Chikonji A, hadi Jangwani. Kuhusu barabara ile ya Likotwa kwenda Jangwani hadi yenye urefu wa kilometa 16 tayari kazi ya kuchonga imeanza," alisema Wahabu.
Alisema anamatarajio makubwa kwamba miundombinu ya barabara itaboreka. Nikutokana na mipango mizuri ya serikali ya awamu ya sita katika kuongeza vyanzo vya mapato.
Alifafanua kwamba kitendo cha serikali kuweka tozo kwenye mafuta kwa ajili ya TARURA kitasababisha barabara nyingi kujengwa na kufanyiwa matengenezo.
Mbali na hayo mtaalamu huyo wa ujenzi alizitaja baadhi ya changamoto ambazo kwa kiasi fulani zinakwamisha utekelezaji wa miradi kuwa ni pamoja na idadi ndogo ya watumishi ambayo halingani na mahitaji, vitendea kazi hasa magari kwa ajili ya usimamizi.
Kwani magari mengi yamechakaa. Huku akiweka wazi kwamba kwasasa wanashughulikia sehemu korofi.
Kuhusu idadi ndogo ya watumishi alisema mahitaji halisi kwa mujibu wa muundo wa utumishi ilitakiwa wawepo watumishi 16.
Hatahivyo ofisi yake inawatumishi wanne tu.
