Waziri wa Afya, Maendeleoa ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima,amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za mapitio ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003,ili kutimiza azma ya kuimarisha afua mbalimbali kwa wazee nchini.
Kauli hiyo ameitoa leo September 6,2021 Wilayani Manyoni Mkoani Singida alipotembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza ya Sukamahela kuelekea Siku ya Wazee Duniani Okotoba 1.
Waziri Dkt Gwajima amesema serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza afua mbalimbali zinazalenga katika kutatua changamoto mbalimbali zinazaowakabili wazee
“Katika sera hiyo ikiwemo huduma za afya, matunzo, ulinzi na usalama, hifadhi ya jamii, maandalizi ya wananchi kuelekea maisha ya uzee na msaada wa kisaikolojia yamewekewa mikakati madhubuti ili kuhakikisha wazee wanapata huduma jumuishi na stahiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao,”amesema
Amesema sherehe za maadhimisho ya siku ya wazee mwaka huu zitaambatana na huduma mbalimbali ikiwemo kupimwa maradhi mbalimbali kama vile presha, kisukari na tezi dume.
Dk. Gwajima alisema pia zitatolewa huduma za msaada wa kisaikolojia na elimu kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na kuhamasisha wazee na wananchi kupata chanjo.
“Sherehe za maadhimisho ya siku ya wazee itahusisha huduma mbalimbali kama vile wazee kupima presha, kisukari, tezi dume, huduma za msaada wa kisaikolojia na elimu kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuhamasisha wazee na wananchi kupata chanjo.” amesema Dkt Gwajima
Hata hivyo amesema kuwa Lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala mbambalimbali ya wazee ikiwa ni pamoja na kutafakari fursa na changamoto zinazo wakabili na namna ya kuzitatua.
“Hivyo ni wajibu wetu kama taifa kutumia siku hii kutambua machango wa wazee na kuwaenzi ipasavyo kwa kulinda, kuhifadhi, kukuza na kuimarisha upatikanaji wa haki zao katika jamii”alisisitiza Dk. Gwajima
Waziri Gwajima amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika ngazi za mikoa na maeelekezo tayari yametolewa kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI.
Waziri Dkt Gwajima ameiagiza mikoa ya Rukwa na Njombe kuunda Mabaraza ya Wazee ya Mikoa hiyo ili kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la Wazee litakalosaidia kuleta wazee pamoja katika mijadala mbalimbali na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Awali akisoma taarifa ya Makazi ya Wazee Sukamahela Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo Twaha Kibalula amesema kuwa Makazi hayo yanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari kwa ajili ya kutoa huduma kwa Wazee hao ikiwemo huduma za kiafya zinazopatikana kwenye hospitali za Wilaya na Mkoa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Rahabu Mwigwisa amemshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa kuwatembelea Wazee hao na amemuhakikishia kuwa Wilaya itaendelea kuwaangalia kwa ukaribu Wazee hao kwani ni tunu kwa Taifa hivyo itahakikisha wanapata huduma zote stahiki.
Naye Mwenyekiti wa Wazee hao Mzee Adrea Yohana amemshukuru Waziri Dkt Gwajima na Serikali kwa ujumla kwa huduma wanazozipata na kumuomba kuendelea kuboresha huduma za afya, chakula na malazi ili waweze kuishi kwa amani na furaha zaidi.



