Marekani na Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuchukua hatua inayolenga kupunguza kwa thuluthi moja uzalishaji wa gesi chafu inayoharibu mazingira inayosababisha ongezeko la joto duniani.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizoonekana na shirika la habari la Reuters, hatua hiyo itachukuliwa kufikia mwishoni mwa muongo huu na nchi hizo zinatoa msukumo kwa nchi nyingine kubwa duniani kujiunga na harakati hiyo.
Makubaliano hayo yanakuja wakati Marekani na Umoja wa Ulaya zikitaka kuzishawishi nchi nyingine kubwa kiuchumi kabla ya mkutano wa kilele wa dunia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi utakaofanyika mjini Glasgow,Scotland mwezi November,kuchukua hatua hiyo.
Hatua ya Marekani na Umoja wa Ulaya inaweza kuwa na athari muhimu kuelekea nishati,kilimo na viwanda vya takataka ambavyo ndivyo vinavyozalisha kiwango kikubwa cha moshi unaochafua mazingira.
Katika hatua ya kujaribu kuanzisha mpango huo wa kupunguza viwango vya gesi chafu,baadae wiki hii Marekani na Umoja wa Ulaya zitatoa ahadi ya pamoja ya kupunguza uzalishaji huo kwa alau asilimia 30,kufikia mwaka 2030.
