Serikali
kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini imekamilisha mwongozo wa
kitaifa wa kuwawezesha wahitimu wa kada za afya ambao hawana ajira
rasmi, waweze kuajiriwa kwa muda.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima wakati akifungua
Mkutano Mkuu wa mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri mjini
Dodoma.
Dkt. Gwajima,
amesema, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wamekamilisha mwongozo
wa Kitaifa wa Kujitolea (National Health Workforce Volunteerism
Guideline) unaotoa utaratibu wa namna bora ya Hospitali na Vituo vya
afya kutumia wahitimu wa kada ya afya ambao hawajaajiriwa ili waweze
kutumika rasmi katika utoaji wa huduma za afya kwa njia ya kujitolea.
“Mwongozo
huo ni mkakati mahususi wa kuboresha huduma za afya kwa kukabiliana na
uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya nchini hii hapa ikiwa ni pamoja
na kuongeza wigo wa upatikanaji na utoaji wa huduma bora za Afya kwa
wananchi” amesema Waziri Gwajima.
Waziri
Gwajima, amesema, Serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza Afua
za Sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 2,726 wa kada za
Afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, lengo likiwa ni kuikamilisha
utoaji wa huduma za afya nchini.
Katika
hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema Mkutano huo ambao umebebwa na
kaulimbiu isemayo Ustahimilivu wa Mifumo ya Afya katika Mapambano dhidi
ya UVIKO-19; ‘changamoto na fursa’ unatoa ishara ni kwa namna gani
wataalam wa afya wanavyoshirikiana kutekeleza majukumu yao wanapo
kabiliana na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (UVIKO -19) tokea ulipoingia
hapa nchini.
“Pamoja na
changamoto zilizopo, mmeendelea kujitoa na kutumia weledi wenu katika
kuihudumia jamii, hili ni jambo la kizalendo, hongereni sana, nichukue
nafasi hii kuwaelekeza viongozi wote wa ngazi zote kushiriki
kuwahamasisha wananchi kwenda kupata chanjo ya UVIKO -19 kwani chanjo
hizo ni Salama, amesisitiza Dkt. Gwajima.
Kwa
upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange,
amesema serikali kuanzia awamu ya tano na ya sita zimekuwa zikitoa
kipaumbele katika huduma za fya, ambapo katika mwaka fedha wa 2021/22,
jumla ya Hospitali 28 zinakwenda kuanza ujenzi wa Hospitali za Wilaya
ambazo hazikuwepo kabisa, aidha Tarafa zote 207 zitajengewa Vituo vya
afya huku Tarafa 150 zikiwa tayari zimeshapelekewa fedha katika mwanzo
wa mwaka kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Dkt.
Dugange Amewakumbusha Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri, kusimamia
ipasavyo rasilimali zote zinazofika kwenye maeneo yao huku akiwataka
kutumia Mkutano huo kama sehemu ya darasa la kujifunza katika
kukabiliana na Uviko-19 kwa kubadilisha uzoefu kutokana na changamoto
kutofautiana.
Akitoa
salaam za Wizara ya Afya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel
Makubi, amehimiza suala la uimarishaji wa utoaji wa huduma kwani Pamoja
na kujenga miundombinu lakini saula la msingi ni uimarishaji wa utoaji
huduma za afya, amesema watoa huduma lazima wawe na lugha zisizo za
kumkera mtu anayepatiwa huduma.
Naye
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, yeye
amewataka Waganga wakuu wa Mikoa kuwa mstari wa mbele katika suala la
kuchanja, aidha Wizara itafatilia kujua Mkoa na Halmashauri kinara
katika zoezi la kuchanja chanjo ya Uviko-19.
Mapema
akiongea katika Mkutano huo, Dkt. Florence Temu, kutoka AMREF na
mwakilisi wa Non state Actors, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa
juhudu kubwa zinazo chukuliwa katika mapambano dhidi ya Uviko-19, na
kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali.
“Awali
kulikuwa na vituo vya kutolea huduma za chanjo 500 lakini kwa takwimu
za sasa inaonesha idadi ya vituo hivyo imeongezeka na kufikia 1500, hii
ni hatua kubwa, tunaimani Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa
wadau lakini pia kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za Uviko-19.
Amesema Dkt. Florence.