Oct 13, 2021

Rais Samia Kinara kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma kiuchumi - Dkt.Gwajima

  Muungwana Blog 2       Oct 13, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara na kuweka ahadi katika kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma katika usawa wa Kijinsia na uwezeshaji kiuchumi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati akiongea na waandishi wa habari nchini hapa kwenye Kongamano la tatu la wanawake nchini Urusi


Dkt. Gwajima amesema kuwa Mhe. Rais  tangu aingie madarakani ameweka ahadi ya kuhakikisha anayatazama masuala ya wanawake, haki zao na masuala ya usawa wa kiuchumi ili wasiachwe nyuma kwa sababu ya ajenda ya kijinsia ambayo huwaweka pembeni na kushindwa kuchangia maendeleo ya Taifa lao.

“Rais Samia amekuwa  kinara na ameona ni vyema Tanzania tuje kusikia, kuona na kujifunza ili tusiachwe nyuma katika ajenda za kuwaendeleza wanawake  na kuwa na maendeleo chanya katika nchi yao”. alisema Dkt Gwajima

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa, wanawake Afrika ndio wanachangia sehemu kubwa ya kufanya muonekano wa Taifa na ni walezi wa familia hivyo kongamano hilo ni muhimu katika ajenda ya kuwaendeleza wanawake hususan wanawake wa Kitanzania.


Amesema pia Kongamano la tatu la wanawake litaangalia mustakabari wa wanawake duniani katika kupewa haki na fursa sawa za kuendelea kiuchumi ili waweze kuchangia maendeleo chanya katika jamii zao.

Vile vile Dkt. Gwajima ametumia fursa hiyo kuishuruku nchi ya Urusi kwa ushirikiano na Tanzania kwa takribani miaka 60 iliyopita kwa kusaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo kusomesha wataalam si chini ya 4500 katika fani mbalimbali akiwemo yeye mwenyewe Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto.

Tanzania inashiriki Kongamano la tatu la Wanawake Urusi ambapo Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Sulluhu Hassani.

 

logoblog

Thanks for reading Rais Samia Kinara kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma kiuchumi - Dkt.Gwajima

Previous
« Prev Post

No comments:

Post a Comment