https://monetag.com/?ref_id=TTIb Wakuu wa mikoa, wakurugenzi wapigwa 'stop' kutoka nje ya mikoa yao | Muungwana BLOG

Wakuu wa mikoa, wakurugenzi wapigwa 'stop' kutoka nje ya mikoa yao

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu amewapiga marufuku wakuu wa mikoa na wakurugenzi kutoka nje ya mkoa bila kibali cha Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.

Ummy amesema hayo leo Jumanne Oktoba 12, 2021 katika mkutano wa waandishi wa habari akifafanua Tamisemi itakavyotumia mkopo wa IMF kutekeleza miradi mbalimbali ambayo utekelezaji wake unawahusu viongozi na watendaji hao wa mikoa nchini.

Amesema kuwa wakuu wa mikoa na wakurugenzi wanatakiwa kuepuka safari zisizo za lazima za kutoka nje ya mkoa isipokuwa kwa kibali cha viongozi hao.

 “Lakini kwa sababu tunajambo hili kubwa, ninawaelekeza viongozi wote wa Serikali ndani ya Tamisemi, ngazi ya mikoa, wilaya na halmashauri kuepuka safari zisizo za lazima zinazohusu kutoka nje ya mkoa wako isipokuwa kwa kibali cha viongozi wakuu wa nchi."

“Kwa hiyo mkuu wa mkoa ukitaka kutoka ndani ya Mkoa wako kipindi hiki lazima upate kibali cha rais, kibali cha Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.

Tunataka wabaki katika mikoa yao,  tunataka wasimamie utekelezaji wa miradi hii hata mimi waziri wa Tamisemi kama nitawaita maana yake lazima nipate kibali cha rais au waziri mkuu, makamu wa rais cha kusema waziri nimekuruhusu uwaite wakuu wa mikoa, wakurugenzi watoke ndani ya halmashauri zao," amesema Ummy.

 

Post a Comment

0 Comments