Na John Walter- Manyara
Wazee wa Kimila katika kata ya Ayalagaya
wilayani Babati mkoani Manyara wamewapiga faini ya kulipa ng'ombe dume
watatu kwa kosa la kuingia kijijini hapo na kuanza kufanya kazi kwenye
chanzo kilichopo kijijini hapo bila kutoa taarifa kwao.
Wazee hao
wametoa tamko hilo mbele ya mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro
oktoba 11,2021 alipofanya ziara yenye lengo la kufanya upatanisho kati
ya viongozi wa wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira mjini
Babati (BAWASA) na wakazi wa vijiji vya Ayalagaya, Haysam na Gajal kwa
madai ya mafundi wa BAWASA kuharibu chanzo cha maji katika mto Endalo na
kusababisha maji kukosekana kwa siku saba.
Akitoa maelezo mbele ya
mkuu wa mkoa Diwani wa Kata ya Ayalagaya Sabini John alimwabia mkuu wa
mkoa kwamba, Mafundi hao waliingia kwenye chanzo kinachotumika na wakazi
wa vijiji hivyo na kuanza kufanya shughuli za kutaka kusambaza maji
katika vijiji vingine bila elimu kutolewa kwa wakazi wa vijiji husika.
Bw.
John alieleza kuwa, mafundi hao bila taarifa walisababisha maji
kuchafuka kwa kuchan’ganywa na saruji kitendo kilichowafanya vijana
kuelekea sehemu ya chanzo hicho na kuwakuta mafundi hao ambao
walichukuliwa hadi ofisi ya kijiji kwa kuchukuliwa maelezo ambayo
hayakupokelewa hadi mkuu wa Wilaya Babati Lazaro Twange kuingilia kati.
“Mafundi
waliingia msituni kwenye chanzo bila kusaini kwenye ofisi ya kijiji,
vijana waliopandisha kwenye chanzo na kuwakuta walikuwa wastaarabu sana
kwani hawakuwafanyia fujo yoyote zaidi ya kuwafikisha ofisini salama na
hatimae kuwaruhusu waende hadi mwafaka upatikane” alisema.
Aidha mkuu
wa mkoa alipokutana na wananchi wa vijiji hivyo jambo la kwanza
aliwaruhusu watoe kero zao kwanza ndipo naye aweze kutoa majibu ya hoja
zao bila kuathiri upande wowote na kuweza kupata muafaka wa yaliyotokea
na kusababisha taharuki kwa wakazi hao.
Baada ya maelezo ya pande
mbili kutolewa mbele ya mkuu wa mkoa huo ilionekana mafundi wa Bawasa
walikuwa wakifanya shughuli zao bila kuwashirikisha viongozi wa kata
husika ya Ayalagaya.
Akiongea kwa niaba ya wazee walioshiriki mkutano
huo wa mkuu wa mkoa mzee Michael Tsaghara aliuambia mkutano kuwa,
mafundi wameomba msamaha, hivyo wazee wamesema msamaha utakubalika
endapo watalipa faini ya kulipa madume watatu wa ng’ombe watakaochinjwa
na kuliwa hapo kwenye uwanja wa mikutano.
Mafundi hao wakiongozwa na
Mhandisi Rashidi Cherehani wameridhia kulipa faini hiyo na tayari wako
sokoni wakiwasaka madume hao watatu watakaowasilishwa uwanjani tayari
kwa kitoweo cha wazee wa kata nzima na majirani zao.