Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amesema kuwa serikali yake haitaki ugomvi na Poland bali inautaka Umoja wa Ulaya kuwachukua wahamiaji 2,000 waliokwama kwenye mpaka wake.
Kauli ya Lukasheko imekuja baada ya Poland kuonya leo kuwa mivutano kuhusu watu hao waliokwama mpakani huenda ukalipuka na kuwa janga kubwa. Lukashenko amenukuliwa na shirika la habari la serikali Belta akisema anafahamu vyema hali iliyopo sasa na hataki mzozo huo uwe mbaya zaidi.
Umoja wa Ulaya unaituhumu Belarus kuwa inawasafirisha maelfu ya watu kutoka Mashariki ya Kati na kuwashinikiza kuingia Umoja wa Ulaya kupitia Poland, Lithuania na Latvia kama njia ya kulipiza vikwazo vya Ulaya.
Belarus inakanusha kuhusika na mzozo huo wa uhamiaji. Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki ameonya kuwa mzozo huo wa uhamiaji mpakani ni kama jaribio kubwa la kuiyumbisha Ulaya tangu enzi ya Vita baridi