Serikali ya Nicolas Maduro, ambaye ushindi wake wa uchaguzi wa 2018 haujatambulika na sehemu ya jamii ya kimataifa, imeshinda kwa kishindo uchaguzi wa jana wa serikali za majimbo, ambao ulivishirikisha vyama vya upinzani nchini Venezuela kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2017.
Uchaguzi huo wa nyadhifa za gavana na meya, na ulioshuhudiwa na waangalizi wa Umoja wa Ulaya waliorejea nchini humo baada ya miaka 15, ulikuwa mtihani muhimu kwa serikali ya Maduro katika nchi iliyoharibiwa vibaya kwa vikwazo vya kimataifa na mgogoro wa kiuchumi.
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya utatoa ripoti yake kesho. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema asilimia 41.8 ya wapiga kura walijitokeza, ambapo watu milioni 8.1 kati ya wapiga kura milioni 21 walipiga kura yao. Wagombea wanaoegemea upande wa Maduro walipata nyadhifa 20 kati ya 23 za ugavana na umeya wa mji mkuu Caracas.