Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Faida na hasara ya kuwa na uzoefu katika jambo fulani

 

Ingawa uzoefu ni kitu kizuri ambacho watu wengi wanatamani kuwa nacho,unaweza kuwa na uzoefu ukakusaidia au ukapelekea kupata hasara katika maisha kutokana na namna unavyoutumia.

Kuna watu wengi ambao wamefanikiwa kupata nafasi nzuri za kazi kutokana na uzoefu waliokuwa nao, na wengine licha ya kuwa na vyeti vizuri sana vya taaluma wamekosa fursa za kuajiriwa kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu.

Uzoefu ni nini?
Kitu hiki uzoefu kinafafanuliwa kuwa ni maarifa, elimu au uelewa fulani ambao mtu anakuwa nao kutokana na kufanya kazi katika eneo fulani kwa muda mrefu. Uzoefu ni kitu ambacho hakishikiki kinakaa ndani ya mtu. Ili kumpima mtu kama ana uzoefu si kutokana na anavyosema ila namna mtu huyo anavyouweka huo uzoefu kwenye matendo kusaidia maisha yake na kupunguza changamoto katika jamii.

Uzoefu unaweza kuambatana na cheti cha taaluma au mtu anaweza kuwa na uzoefu hata kama hana cheti chochote cha taalum. Miaka ya nyuma hapa Tanzania kulikuwa na watu waliofanya kazi za kihandisi bila kuhudhuria elimu yoyote ya darasani kutokana na uzoefu waliojenga kwa muda mwingi wakiwa kazini.

Watu wa namna hii walifanya vizuri sana kwenye kazi wakati mwingine kuliko hata wahandisi waliokuwa wameajiriwa mara tu baada ya kumaliza masomo yao ya shahada za uhandisi,kwa nini? Kwa sababu hawa walikuwa na vyeti bila uzoefu wowote na hawa hawakuwa na cheti chochote lakini walifanya vizuri.

Ninachotaka kukumbushana kupitia makala hii ni namna gani mtu anaweza kunufaika kutokana na uzoefu alionao iwe uzoefu chanya au hasi, wakati huo huo mwingine anaweza asinufaike kwa namna yoyote kutokana na uzoefu wake.

Uzoefu ni mchanganyiko wa mambo yote mazuri na mabaya ambayo mtu amepitia na kufanya katika maisha yake.Haliwezi kuwa swala la upande mmoja tu,lazima uwe na sura yenye pande mbili. Ukikuta mtu anajinadi kuwa na uzoefu wa kufanya vizuri,au ana uzoefu wa kufaulu tu huyo anaweza kuwa bado hajafuzu darasa la uzoefu.

Ukweli kuhusu maisha dunia tunayoishi imejengwa na watu wa aina mbili wanaofanikiwa na wale ambao hawafanikiwi,na watu wote hawa ni muhimu sana dunia inawahitaji wote kutokana na mchango wao.

Watu wengi hupenda kusimulia namna walivyofanikiwa lakini habari muhimu ambayo inaweza kuvuta masikio ya wasikilizaji na macho ya wasomaji wengi siyo hadithi ya mafanikio ila kushindwa na uliposhindwa ulifanya nini akainuka tena na kuwa miongoni mwa washindi.

Kama kuna watu wamewahi kushindwa katika maisha ni wale ambao leo unaona wamefanikiwa. Ni rahisi kufikiri kuwa wanaoonekana kufanikiwa leo waliibuka wakiwa washindi tu hapana,chukua nafasi ya kujifunza utashangaa. Kila mshindi nyuma yake kuna hadithi ya kushindwa.

Kinachotofautisha mtu anayefanikiwa na yule ambaye hafanikiwi ni namna wanavyopokea hakuna uzoefu unaoweza kumzuia mtu anaefanikiwa kushindwa kufikia hatma anayokusudia. Wakati yule mwenye mtazamo wa kushindwa anakata tamaa pale anapokutana na magumu mwenye mtazamo wa kushinda huchukulia kushindwa kama sehemu ya mchakato kuelekea ushindi.

Namna gani mtu anaweza kupata hasara au faida kutokana na uzoefu?
Hapa kuna watu wawili wenye uzoefu wa aina mbili unaofanana,tofauti yao ni namna wanavyopokea na kutumia huo uzoefu. Mtu anayeelekea ushindi na yule anayeelekea kushindwa wote wamebeba ndani mwao uzoefu wa kushinda na ule wa kushindwa.

Hofu ya kuogopa kushindwa ni jambo ambalo limepelekea watu wengi kushindwa kufikia malengo yao.Hali hii husababisha watu kushindwa kuchukua hatua kuelekea kule wanakotaka kutokana na aina fulani ya uoga ndani mwao. Uzoefu walio nao huwakumbusha jinsi wao wenyewe walivyowahi kushinwa,au ndugu na marafiki zao walivyoshindwa.

Hebu fikiri mtu ameanzisha biashara na kuwekeza kiasi cha kutosha cha fedha aliyokuwa nayo akitegemea kupata faida kubwa. Matokeo yake biashara inakwenda mlama na kujikuta anapata hasara kwa kupoteza karibu mtaji wake wote aliowekeza. Hali hiyo inapelekea mtu huyo kushindwa kufanya kitu chochote kwa uoga uliosababishwa na hasara ya biashara aliyojaribu mara moja. Hadithi ya kushindwa inachukua nafasi katika maisha yake yote.

Uzoefu kama huu huleta matokeo ya hasara katika maisha ya mtu na pengine maisha yake yote. Hasara kubwa anayopata mtu wa namna hii siyo mtaji aliopoteza kwenye jaribio la biashara isipokuwa hasara ya kufunga milango yote ya uwezekano iliyo mbele yake.

Hawezi kujua kama uliofungika ulikuwa ni mlango mmoja tu na bado iko milango mingi ya uwezekano wa kufanikiwa na kurudisha fedha yake yote ambayo hata hajaiguswa. Sasa tofauti ya anayepata hasara na yuele anayepata faida kutokana na uzoefu ni ipi?

Anayeshinda yeye haogopi kushindwa;
Pale mambo yanapotokea kinyume na jinsi walivyotegemea watu wanaotazama ushindi hawachukulii hali hiyo kama kikwazo cha kuwafanya wasiende mbele.Badala yake huchukulia kama sehemu ya mchakato kuelekea ushindi.

Hujiuliza ndio ni kweli nimeshindwa katika jaribio hili la kwanza je! Kuna kitu gani naweza kujifunza kutokana na hali hii ili niweze kufanya vizuri siku za usoni? Je! Nifanye nini ili kuvuka na kusaidia watu wengine kuvuka?

Kwa hiyo akutane na uzoefu mgumu kiasi gani mtu wa aina hii yeye haangalii namna alivyoshindwa badala yake hujielekeza mbele anakoelekea bila kuangalia ajali ambazo amewahi kukutana nazo katika safari yake ya kusaka mafanikio.

Anayeshindwa yeye huogopa kushindwa;
Kutokana na uzoefu aliopitia mtu anayeshindwa yeye hukumbuka kila tukio la kushindwa ambalo amekutana nalo kwenye maisha yake ya safari ya kusaka mafanikio. Anatamani kufanikiwa lakini kikwazo kikubwa kinakuja kuwa ni uzoefu aliokutana nao wa kupata hasara. Kila anapotaka kufanya jambo la msingi hujikumbusha namna alivyopata hasara na kujiambia usithubutu utapata hasara tena.

Hawezi kufanikiwa mtu wa namna hii kwa sababu jinsi tulivyo ni matokeo ya namna tunavyowaza.Tayari mtu kuna namna unavyojiambia na kuanza kuwaza vibaya,na namna unavyowaza vibaya inaumba kujisikia vibaya,na jinsi unavyojisikia vibaya inaumba kutokufanya vizuri.

Hasara au faida kutokana na uzoefu ni mtazamo;
Mtazamo ndicho kitu kinachopelekea mtu kupata hasara au faida kutokana na uzoefu aliokutana nao. Siku zote kuwa katika mtazamo wa ushindi humsaidia mtu kufikia hatima yake hata kama anapita katika vipindi vya changamoto.

Changamoto lazima ziwepo kila siku madhari bado tunaishi. Hatuwezi kushinda kwa kuzikimbia au kuziogopa changamoto badala ya kuzibadilisha ziwe fursa tuzitumie kujiwezesha na jamii inayotuzunguka. Hakuna chochote kinachoweza kukuzuia kuwa chochote unachotaka kuwa.

Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu au email tutapokea na kurudi kwako mapema kadri itakavyowezekana.

Post a Comment

0 Comments