Waziri wa Afya wa Ujerumani Jehns Spahn ameonya leo kuwa ifikapo mwisho wa majira ya baridi kali kila mmoja nchini atakuwa ama amechanjwa, amepona au kufariki kutokana na virusi vya corona. Spahn amewahimiza raia zaidi kuchanjwa dhidi ya Covid-19.
Kansela anayeondoka Angela Merkel ameonya kuwa vizuizi vya sasa vya corona - ikiwemo kuwazuia wasiochanjwa kuingia katika baadhi ya maeneo ya umma havitoshi.
Ameuambia mkutano wa viongozi wa chama chake cha CDU, kuwa hali imekuwa mbaya sana huku maambukizi mapya yakiongezeka maradufu kila baada ya siku 12.
Austria leo imeanza kutekeleza agizo la kuzuia shughuli muhimu za maisha kwa siku kumi kupambana na wimbi la nne la maambukizo.
Ubelgiji na Uholanzi zimelaani vurugu zilizoshuhudiwa katika maandamano ya mwishoni mwa wiki ya kupinga hatua mpya za kupambana na Covid.