Shirika la Umoja wa Mataifa la mipango ya Maendeleo UNDP limesema vita vya Yemen vilivyodumu kwa miaka saba vitagharimu maisha ya watu 377,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Katika ripoti yake, UNDP imesema takriban asilimia 60 ya vifo hivyo vitasababishwa na athari zisizo za moja kwa moja na vita kama vile ukosefu wa maji safi, baa la njaa na magonjwa ilhali vita vyenyewe vitagharimu maisha ya watu wapatao 150,000.
Ripoti hiyo ya UNDP imeongeza kuwa, wengi ambao tayari wamekufa katika vita ni watoto wadogo waliokabiliwa na utapia mlo.
Vita vya Yemen vinaelezwa kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani kote. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la mipango ya maendeleo pia limesema katika ripoti yake kuwa vita vimerudisha nyuma maendeleo ya taifa hilo la Magharibi mwa Asia.